MHE . MWINJUMA KUSHUGHULIKIA MGOGORO WA MAC VOICE NA RAYVANNY

 


Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, amekutana na msanii wa muziki wa Bongo Fleva Mac Voice kwa ajili ya kusikiliza malalamiko yake yanayohusu mgogoro wake na msanii na mmiliki wa lebo ya muziki ya Next Level Music, Rayvanny.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika ofisi za Wizara zilizopo uwanja wa Taifa Dar es salaam  Marchi 6 2026, ambapo Naibu Waziri  amesema Serikali imeanza kuchukua hatua za kulifuatilia sakata hilo ili kupata ukweli wa madai yaliyotolewa na pande husika, huku akiahidi kuwa suala hilo litafanyiwa kazi kwa haraka ili kupatikana suluhisho la haki kwa wahusika.

Mgogoro kati ya Mac Voice na Rayvanny umeibuka baada ya msanii huyo kudai kuwa hakupata malipo ya kazi zake alipokuwa chini ya lebo ya Next Level Music, licha ya makubaliano ya mgawanyo wa mapato yaliyofikiwa wakati wa kusaini mkataba. Sakata hilo limezua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii na miongoni mwa wadau wa muziki nchini. 

Mhe. Mwinjuma amefafanua kuwa Serikali ina jukumu la kuhakikisha haki na maslahi ya wasanii yanazingatiwa, huku akisisitiza umuhimu wa mikataba iliyo wazi na inayolinda pande zote katika sekta ya sanaa.

Kwa upande wake, Mac Voice amemshukuru Naibu Waziri kwa kuonesha nia ya kusikiliza malalamiko yake na kuahidi kuwa ataendelea kushirikiana na mamlaka husika ili suala hilo liweze kupatiwa ufumbuzi.

No comments