Rais Samia Apokea Ripoti ya Maboresho ya Kodi: Mkakati wa "Kuvua Gamba" waandaliwa
Na Mwandishi Wetu, BSKY Media
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepokea rasmi ripoti ya Tume ya Rais ya
Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi nchini, huku akiahidi utekelezaji wa
mapendekezo hayo kwa awamu ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kiuchumi.
Hafla hiyo iliyofanyika Ikulu jijini
Dar es Salaam tarehe 18 Machi, 2026, inaashiria hatua kubwa ya mabadiliko tangu
tathmini ya mwisho ya aina hiyo iliyofanywa na Tume ya Mtei takribani miaka 35
iliyopita (1989–1991).
Mambo
Muhimu Katika Ripoti Hiyo:
- Idadi ya Mapendekezo:
Tume imewasilisha jumla ya mapendekezo 284 ambayo Rais ameahidi
kuwa Serikali itayafanyia kazi kupitia mikakati ya muda mfupi, kati, na
mrefu.
- Ongezeko la Mapato:
Inakadiriwa kuwa utekelezaji wa mapendekezo haya unaweza kuongeza mapato
ya Serikali kwa kiasi cha TZS trilioni 11.025 ndani ya miaka mitatu
ya mwanzo.
- Lengo la Kikodi:
Tanzania inalenga kufikia uwiano wa mapato ya kodi kwa Pato la Taifa
(Tax-to-GDP ratio) wa asilimia 18.
- Dira ya 2050:
Maboresho haya ni sehemu ya maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,
ambapo sekta binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 70 ya mapato.
"Hata
Nyoka Hujivua Gamba"
Akizungumzia ulazima wa mabadiliko
hayo, Rais Samia amesisitiza kuwa mfumo wa sasa unapaswa kubadilika ili uwe wa
haki, usio na tafsiri kinzani, na usioumiza biashara.
"Pamoja na changamoto za mfumo
wa kodi, mabadiliko ni lazima na muhimu. Hata nyoka hujibadilisha, hujivua
gamba. Sisi pia tunapaswa tubadilike," alisema Rais Samia.
Changamoto
Zilizoibuliwa na Tume
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Balozi
Ombeni Sefue, alibainisha kuwa mfumo wa sasa unakabiliwa na changamoto kadhaa
ikiwemo:
- Viwango vikubwa vya kodi na tozo fulani.
- Udhaifu katika utatuzi wa migogoro ya kodi.
- Uratibu hafifu miongoni mwa taasisi zinazokusanya
mapato.
- Wigo mdogo wa walipakodi, hali inayofanya kodi
kukusanywa kutoka kwa watu wachache.
Balozi Sefue alionya kuwa bila
mabadiliko makubwa, nchi itaendelea kukamua maziwa bila "kulisha
ng'ombe," akimaanisha lazima mfumo uimarishe uwekezaji ili uweze kuzalisha
kodi endelevu.

Post a Comment