NI 'NISHANI' YA PAPA KWA RAIS SAMIA: DIPLOMASIA YA MARIDHIANO YAIPIGA 'JABU' DUNIA
Ujumbe mzito wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV, uliosomwa mkoani Simiyu, umetafsiriwa na wachambuzi wa mambo kama nishani ya juu ya kidiplomasia kwa Serikali ya Awamu ya Sita.
Papa kwa kauli yake amepongeza waziwazi ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na Kanisa, akitaja kuwa ni ishara ya dhati ya kutetea amani, haki na maridhiano .
Kauli hii si tu faraja kwa waumini, bali ni pigo la kishindo kwa wanaharakati na wakosoaji wa nje wanaojaribu kuichafua taswira ya Tanzania katika medani za kimataifa, kwani sauti ya Vatican ina uzito wa kipekee katika kupima utawala bora duniani.
Katika muktadha wa siasa za ndani, kauli ya Papa inakuja kama muhuri wa idhini kwa falsafa ya Maridhiano (R4) ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa kiongozi wa kiroho mwenye ushawishi mkubwa kama Papa kutambua jitihada za serikali katika kusimamia amani na haki, inathibitisha kuwa Tanzania imerejea kwenye mstari wa mstari wa mbele wa mataifa yanayoheshimika kwa utu na utulivu. Hii inatoa kinga ya kimaadili dhidi ya propaganda za mtandaoni, ikionyesha kuwa wenye busara duniani wanaona matunda ya utendaji wa serikali yanayolenga kuunganisha jamii badala ya kuibua mifarakano.
Vilevile, kuanzishwa kwa Jimbo Jipya Katoliki la Bariadi na hivyo majimbo kufikia 37 ni ishara ya upanuzi wa huduma za jamii na usimamizi wa karibu wa maendeleo ya watu.
Kanisa Katoliki limekuwa mshirika mkuu wa serikali katika kutoa elimu, afya na maji, hivyo Papa kusifu ushirikiano huo ni kielelezo cha namna serikali inavyotengeneza mazingira wezesha kwa taasisi za dini kutekeleza majukumu yao.
Uhusiano huu unajenga msingi imara wa siasa za kimaendeleo ambapo dini na dola zinashirikiana kwa maslahi ya mwananchi wa kawaida, bila kuingiliana katika misingi ya kiutawala.
Hata hivyo, ujumbe huo umebeba onyo la kiadilifu lililotolewa kupitia Askofu Severine Niwemugizi, aliyesisitiza kuwa ushirikiano huo usitumike kuficha uovu. Hapa ndipo unapoonekana ukomavu wa demokrasia nchini; ambapo kanisa linabaki kuwa "dhamira ya taifa" likiikumbusha serikali na viongozi wake kutotafuta utukufu wa wanadamu bali kutenda haki.
Katika siasa za Tanzania, kauli hii inaimarisha dhana ya uwajibikaji, ikionyesha kuwa serikali inayokubalika na Papa ni ile inayopokea sifa kwa yale yaliyonyooka, huku ikibaki tayari kusikiliza sauti za kinabii pale changamoto zinapojitokeza kwa ustawi wa taifa.

Post a Comment