KIPA WA ZAMANI STARS ABARIKI KIKOSI, ASIFU MANULA KUREJEA KIKOSINI
KIPA wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars, Steve Nemes, ametoa utabiri wa mafanikio kuelekea michezo ijayo ya kimataifa, akisema kikosi kilichotajwa hivi karibuni kina uwezo mkubwa wa kutoa matokeo chanya.
Nemes amepongeza uamuzi wa benchi la ufundi kumrejesha kipa mzoefu Aishi Manula, akibainisha kuwa hatua hiyo inaongeza hali ya kujiamini na utulivu katika safu ya ulinzi ya Stars kuelekea michuano ya FIFA Series 2026 itakayofanyika jijini Kigali, Rwanda.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Nemes amefafanua kuwa kurejea kwa Manula ni jambo la kimkakati kutokana na uzoefu wake wa miaka mingi katika kiwango cha juu.
Alieleza kuwa kipa huyo siyo tu anakwenda kuwania nafasi ya kudaka, bali atakuwa na jukumu la ziada kama ‘mwalimu’ wa makipa chipukizi kikosini. Uwepo wa Manula unatarajiwa kuwa chachu ya mafunzo na kuongeza nidhamu kwa makipa wanaochipukia, jambo ambalo litasaidia kujenga misingi imara ya baadae katika nafasi hiyo muhimu.
Nemes pia aligusia kurejea kwa kipa mwingine mzoefu, Yona, akisema kuwa ushindani wa namba ndani ya kikosi ndiyo siri ya mafanikio ya timu yoyote ya taifa inayotaka kushindana kimataifa.
Alihimiza benchi la ufundi kuendelea na mfumo wa kuchanganya wachezaji wenye uzoefu na damu changa ili kupata uwiano mzuri (balance) utakaohimili mikiki ya mechi za kirafiki za FIFA, ambazo ni kipimo muhimu kabla ya kuingia katika mashindano makubwa rasmi.
Katika kutoa rai kwa wachezaji walioitwa kambini , kipa huyo wa zamani amewataka kuzingatia nidhamu ya hali ya juu na kufuata maelekezo ya makocha kwa usahihi.
Alisisitiza kuwa kila mchezaji anapaswa kutambua thamani ya jezi ya taifa na kutumia mechi hizo za kirafiki kama jukwaa la kuthibitisha ubora wake. Kwa mujibu wa Nemes, michezo hiyo ya Kigali ni fursa adhimu kwa timu kufanya majaribio ya mifumo mbalimbali na kuimarisha muunganiko wa wachezaji ili kuifanya Stars kuwa tishio zaidi.

Post a Comment