BAKWATA YAHIMIZA MALEZI BORA, MARIDHIANO NA ULINZI WA AMANI
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limetoa wito mzito kwa wazazi, walimu na viongozi wa dini kuungana pamoja katika kuboresha malezi ya watoto na kulinda umoja wa kitaifa.
Akizungumza Machi 21, 2026, katika Baraza la Idd el-Fitr lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa BAKWATA Taifa, Alhaj Nuhu Mruma, ameeleza kuwa malezi bora yanahitaji mshikamano wa wadau wote.
Alibainisha kuwa jamii ikisimama pamoja katika kulea watoto kwa maadili mema, itasaidia kuondoa changamoto za mmomonyoko wa maadili na kujenga taifa imara lenye ustawi.
Chini ya kauli mbiu isemayo "Amani na Maadili Mema katika Kujenga Jamii Bora," BAKWATA imetangaza kampeni maalum ya kurudisha maadili na uzalendo, hususani miongoni mwa vijana wanaokumbwa na changamoto za mitandao ya kijamii.
Alhaj Mruma amewaomba wazazi na walezi kudhibiti athari za kidijiti kwa vijana, huku akishauri serikali kuboresha mitaala ya elimu ili iguse masuala ya malezi na uzalendo.
Alisisitiza kuwa viongozi wa dini zote wanapaswa kuwa daraja la kuunganisha taifa na kuepuka hila zozote zinazoweza kusababisha mpasuko, wakitumia nafasi zao kuwajenga waumini katika upendo badala ya kuwa kichocheo cha vurugu.
Aidha, Katibu Mkuu huyo ametoa wito kwa Watanzania kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuleta maridhiano ya kweli nchini.
Alipongeza uamuzi wa Serikali kuunda Tume maalum ya kuchunguza matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29 mwaka jana, akisema kuwa matukio hayo yalichafua taswira ya nchi.
Alieleza imani ya waumini kuwa Tume hiyo itatoa majibu ya haki yatakayoponya vidonda vya kijamii, huku akiwahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa Tume hiyo katika siku zake chache zilizobakia ili kukamilisha kazi hiyo muhimu.
Alhaj Mruma pia amevishukuru vyombo vya usalama kwa kufanya kazi ya ziada kurejesha utulivu nchini kwa muda mfupi baada ya vurugu za Oktoba 29.
Alihitimisha kwa kuwataka Watanzania kuchukua funzo kutokana na yaliyotokea ili kuepuka mifarakano inayoweza kuhatarisha amani na mali za wananchi, akisisitiza kuwa amani ndiyo mtaji mkuu wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Baraza hilo lililohudhuriwa na Rais Samia kama mgeni rasmi, limepambanua nafasi ya BAKWATA kama mdau muhimu wa amani na mshikamano katika ujenzi wa jamii bora ya Kitanzania.
Post a Comment