Tanzania yatinga fainali pooltable Afrika
TIMU ya Taifa ya Tanzania mchezo wa Pooltable imefanikiwa kutinga fainali ya mashindano ya Afrika kwa kuifunga Zambia kwa fremu 13-9 kwenye mashindano yanayofanyika Durban Afrika Kusini.
Kwa matokeo hayo sasa Tanzania itacheza dhidi ya wenyeji Afrika Kusini fainali ambayo itakuwa ni marudio ya fainali ya 2023 ambapo Tanzania ilipoteza kwa fremu 11-13.
Katika mashindano hayo Tanzania iliifunga Zimbabwe kwa Fremu 14-11, Afrika Kusini kwa fremu 13-12, Kenya kwa 13-12 na mchezo wa kwanza Tanzania ilifungwa na Botswana kwa fremu 18-7.
Akizungumza Mwenyekiti wa Chama cha Pool Tanzania (TAPA), Wilfred Makamba alisema morali ya timu iko juu na wanatarajia kulipa kisasi kwani wamedhamiria kuwania ubingwa mwaka huu.
"Ushindani ni mkali, lakini timu yetu imejiandaa vyema kuonesha ustadi wetu kwenye fainali. Lengo letu ni kufanya vizuri na kufikia malengo tuliyojiwekea," alisema Makamba.
Kwa upande wa timu ya Taifa ya wanawake ya Tanzania ilifungwa na Afrika Kusini kwa fremu 15-4, mchezo wa kwanza ilipata ushindi dhidi ya Botswana kwa kuifunga kwa fremu 13-12, na baadae ikapoteza mbele ya Zimbabwe kwa fremu 16-9.
Wakati huo huo Mtanzania Jackson Ng’anyi amefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya mchezaji binafsi kwa pooltable kwa kumfunga Mtanzania mwenzke Omary Akida hatua ya robo lakini alipoteza nusu fainali mbele ya bingwa wa Afrika Kusini Harry Martin baada ya kufungwa kwa fremu 3-7 na sasa anasubiri kucheza mchezo wa kumpata mshindi wa tatu dhidi ya Lutham Banda ambaye amepoteza dhdi ya Shaun Martheze.
Mchezaji wa timu ya Tanzania wanawake Cecilia Kileo amepata ushindi wa fremu 4-2 dhidi ya Doreen Wandia wa Kenya.
Jumla ya washiriki 38 walishiriki katika kipengele hicho cha wachezaji binafsi ambapo kwa timu mfumo uliotumika kwa wanawake na wanaume ni mfumo wa ligi.

Post a Comment