TIMES CHOGO ANYAKUA URAIS GOFU WANAWAKE



Chama cha Gofu cha Wanawake Tanzania (TLGU) kimeingia katika awamu mpya ya uongozi kufuatia kukamilika kwa uchaguzi mkuu uliofanyika , Februari 21, 2026, katika ukumbi wa klabu ya gofu ya Lugalo jijini Dar es Salaam. 

Uchaguzi huo uliowavuta pamoja wanachama na wadau wa mchezo wa gofu kutoka maeneo mbalimbali nchini, umelenga kupata timu thabiti itakayochochea maendeleo ya mchezo huo na kuimarisha ushiriki wa wanawake katika nyanja za ushindani kitaifa na kimataifa.

Katika matokeo yaliyotangazwa mara baada ya zoezi la upigaji kura, Times Chogo ameibuka mshindi wa nafasi ya Rais wa TLGU, na atasaidiwa na Ayne Ostia Magombe ambaye amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti, huku nafasi ya Katibu Mkuu ikienda kwa Elianasoe Joseph Vitaly ambaye atakuwa na jukumu la kuratibu shughuli za kila siku za chama hicho.

Uongozi huo mpya pia umeimarishwa katika idara ya fedha na ufundi, ambapo Jennifer Nabora Hillar amechaguliwa kuwa Mweka Hazina, huku Chiku Elias Tairo akiaminiwa kushika nafasi muhimu ya Katibu wa Handicap. Timu hii mpya inabeba dhamana ya kusimamia viwango vya wachezaji na kuhakikisha mfumo wa uendeshaji wa mashindano unakuwa na tija kwa maendeleo ya vipaji vya wanawake nchini.

Kwa mujibu wa instagram ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) uchaguzi huu unatazamwa kama hatua muhimu katika kukuza mchezo wa gofu nchini, kwani unakuja wakati kukiwa na uhitaji mkubwa wa kuongeza idadi ya wanawake wanaoshiriki mchezo huo kuanzia ngazi ya vilabu. 

Viongozi hao wapya wana kazi kubwa ya kuendeleza juhudi za kukuza vipaji, kuandaa mashindano mengi zaidi, na kuhakikisha kuwa Tanzania inazidi kupata mafanikio katika mchezo wa gofu kwa upande wa wanawake, huku wakidumisha mshikamano na umoja miongoni mwa wanachama wa chama hicho.

No comments