KIKWETE AMLILIA KARDINALI PENGO: "ALIKUWA RAFIKI WA WENGI NA MTUMISHI WA TAIFA"
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Thaddaeus S. Ruwa'ichi, kufuatia kifo cha Baba Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, akimtaja kama kiongozi aliyetoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi.
Katika barua yake ya rambirambi, Dkt. Kikwete ameeleza kuwa msiba huo ni wa Watanzania wote kutokana na ukweli kwamba wakati wa uhai wake, Kardinali Pengo hakuishia tu kutoa utumishi uliotukuka kwa kanisa lake, bali alijitolea kwa dhati kwa ajili ya maendeleo ya taifa zima.
Kikwete amebainisha kuwa mchango wa Kardinali huyo ulinufaisha Watanzania wengi, wakiwemo Wakristo na wasio Wakristo, hali iliyomfanya kuwa rafiki wa watu wa makundi mbalimbali.
Dkt. Kikwete amesisitiza kuwa Kardinali Pengo atakumbukwa daima kwa moyo wake wa upendo kwa wananchi wenzake na uzalendo wake kwa nchi ya Tanzania. Ameongeza kuwa moyo huo adhimu na mchango wake katika nyanja mbalimbali za kijamii na kitaifa utaendelea kuenziwa kama sehemu ya historia ya mafanikio na mshikamano wa taifa.
Kufuatia msiba huo mzito, Rais huyo mstaafu amewaombea Askofu Mkuu Ruwa'ichi, waumini wa Kanisa Katoliki, na Watanzania kwa ujumla kuwa na moyo wa subira na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na kuomboleza.
Kikwete aliungana na wafiwa kumuombea marehemu mapumziko mema na kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi.

Post a Comment