Castle Lite Unlocks 2026: Mfalme wa Afrobeat, Davido leo 'kuvilipua' viwanja vya Kawe

 


Mfalme wa muziki wa Afrobeat kutoka nchini Nigeria, Davido, anatarajiwa kupanda jukwaani leo usiku katika Viwanja vya Lugalo, Kawe, jijini Dar es Salaam, katika tamasha kubwa la Castle Lite Unlocks.

Davido, ambaye ni mmoja wa wasanii wakubwa zaidi barani Afrika mwenye ushawishi wa kimataifa, atakuwa kivutio kikuu cha usiku huu, huku waandaaji wakithibitisha kuwa maandalizi yote yamekamilika ili kutoa burudani ya kiwango cha juu.

Waandaaji wa tamasha hilo wamethibitisha utayari wao huku wakisema tiketi za VVIP zote zilimalizika kuuzwa rasmi wiki iliyopita, wiki moja kabla ya tukio linalosubiriwa kwa hamu kubwa la Castle Lite Unlocks na Davido.

Tiketi za kiingilio cha kawaida ni shilingi 40,000 bado zinapatikana kupitia tovuti ya www.castlelite.co.tz

Usafiri wa umma kuelekea eneo la tukio unapatikana, na maegesho ya magari ni bure kwa watu watakaohudhuria Castle Lite Unlocks 2026 kwa kutumia usafiri wao binafsi.

Kwa kushirikiana na Idara ya Usalama Barabarani, hatua mbalimbali zimewekwa ili kupunguza usumbufu wa foleni.Watu wanahimizwa kushirikiana magari ili kupunguza msongamano.

Aidha wahudhuriaji wanaonywa kutoleta vitu vyovyote vilivyokatazwa, ikiwemo vitu vyenye ncha kali, aina yoyote ya pombe, vitu vya chuma kama makopo, pamoja na mabango na bendera zenye maudhui yasiyofaa. 

Mashabiki wanahimizwa kufika mapema na wataburudishwa na burudani kutoka kwa wasanii na waburudishaji mbalimbali wakiwemo msanii wa kimataifa, Bontle Modiselle; msanii wa Bongo Fleva Jaivah; wafalme wa Amapiano, Major League DJz; pamoja na mwimbaji mahiri wa Amapiano aliyeshinda tuzo, Mawhoo.

No comments