REGRAGUI ABWAGA MANYANGA MOROCCO



Upepo mbaya umeanza kuvuma ndani ya kambi ya Simba wa Milima ya Atlas baada ya kocha mkuu wa timu ya taifa la Morocco, Walid Regragui, kufikia maamuzi mazito ya kujiuzulu nafasi yake. 

Uamuzi huu umekuja ikiwa ni wiki chache tu tangu timu hiyo iliposhindwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika kufuatia kipigo cha bao moja kwa sifuri dhidi ya Senegal katika mchezo wa fainali. 

Taarifa kutoka nchini Ufaransa kupitia chombo cha Foot Mercato zimebainisha kuwa, Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kifalme la Morocco bado halijatoa tamko rasmi la kukubali au kukataa barua hiyo ya kujiuzulu kwa kocha huyo aliyeweka rekodi za kipekee.

Regragui atakumbukwa kwa kuiongoza Morocco kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo na bara la Afrika kufika hatua hiyo. 

Aidha, aliiongoza timu hiyo kufika fainali ya mashindano ya hivi karibuni ya AFCON yaliyofanyika nchini mwao, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Morocco kuwa mwenyeji tangu mwaka 2004. 

Licha ya kuwa na rekodi bora zaidi kuliko kocha yeyote katika historia ya timu hiyo, Regragui amejikuta akishambuliwa kwa maneno makali na mashabiki pamoja na wadau wa soka nchini humo waliokuwa na matumaini makubwa ya kutwaa taji la Afrika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1976.

Kujiuzulu huku kumekuja katika kipindi ambacho timu hiyo ipo katika maandalizi nyeti ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2026 itakayofanyika nchini Marekani, Mexico, na Canada. 

Wakati shirikisho likitafakari hatua inayofuata, wadau wengi wanahoji kama Morocco itampata mtu sahihi wa kuziba pengo la kocha huyo aliyeweka heshima kubwa duniani.

Mashabiki wa soka nchini humo wamegawanyika, huku wengine wakiona ni muda sahihi wa mabadiliko na wengine wakihofia kuwa kuondoka kwake kunaweza kuyumbisha mikakati ya Simba hao wa Milima ya Atlas kuelekea jukwaa la kidunia mwaka ujao

No comments