KIBANO KIZITO: MC ,DJ BILA VIBALI, FAINI YAKE MILIONI TATU




Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeweka kitanzi kikali kwa Waongoza Sherehe (MCs) na Manju Muziki (DJs) nchini kote kwa kutangaza faini ya papo kwa hapo isiyopungua shilingi milioni moja na isiyozidi milioni tatu kwa yeyote atakayekutwa akifanya kazi bila kuwa na kibali halali. 

Hatua hiyo ambayo imeanza kutumika rasmi tarehe 06 Februari, 2026, inamtaka kila msanii na mdau wa sanaa kusajiliwa na Baraza hilo kwa mujibu wa Kanuni ya 23 (1) ya mwaka 2018, vinginevyo wahusika watakabiliwa na kifungo cha kutojishughulisha na sanaa kwa kipindi kisichopungua miezi sita au kuzuiliwa kabisa kufanya kazi hizo. 

Maelekezo hayo mapya yamebana pande zote mbili kwani hata waajiri au wadau watakaotoa kazi kwa MC au DJ asiye na kibali watachukuliwa hatua kali za kisheria, jambo ambalo limezua taharuki kubwa miongoni mwa vijana wanaojitafuta kupitia tasnia ya burudani.

Licha ya BASATA kusisitiza kurasimisha sekta hiyo kwa lengo la kuwatambua wasanii, wadau wengi wamepiga kelele wakidai kuwa adhabu hizo ni kubwa mno ukilinganisha na hali halisi ya maisha ambapo baadhi ya Ma-DJ wanalipwa mshahara wa shilingi laki moja tu kwa mwezi.

Malalamiko mengi kwenye ukurasa wa instgramu wa Basata yameelekezwa kwenye ugumu wa kupata vitambulisho vya NIDA ambavyo ni hitaji muhimu, huku vijana wakieleza kuwa kushindwa kufanya kazi kutasababisha familia zao kukosa riziki na kuongeza wimbi la uhalifu mitaani. 

Wadau pia wamehoji mantiki ya kutoza mamilioni ya faini kabla ya kutoa elimu ya kutosha mikoani, wakidai kuwa amri hiyo imekuja ghafla bila kuzingatia kuwa wengi wamejiajiri wenyewe kwa vifaa vya mikopo.

Aidha, kumeibuka mjadala mzito kuhusu uhusika wa BASATA katika sherehe za kifamilia na kidini kama harusi, huku baadhi wakihofia kuwa hata shughuli za kijamii zinazofanyika kumbi za starehe sasa zimegeuzwa kuwa chanzo cha mapato ya faini badala ya kutoa huduma kwa jamii.

No comments