MOROCCO YAKATA RUFAA CAF DHIDI YA ADHABU ZA FAINALI YA AFCON 2026
Shirikisho la Mpira wa Miguu la Morocco (FRMF) limetangaza rasmi uamuzi wa kukata rufaa dhidi ya adhabu zilizotolewa na Bodi ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) kufuatia machafuko yaliyotokea kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Fainali hiyo iliyozikutanisha Morocco na Senegal Januari 18, 2026, iligubikwa na matukio ya utovu wa nidhamu ambayo yamepelekea mashirikisho yote mawili kuingia kwenye rungu la CAF.
Katika taarifa yake, Shirikisho la Morocco limebainisha kuwa adhabu zilizotolewa hazilingani na uzito wa matukio yaliyojitokeza uwanjani. FRMF imesisitiza kuwa hatua hiyo ya kukata rufaa imetokana na dhamira yao ya kulinda haki za kisheria za timu yao na wachezaji wake.
Mapema, Kamati ya Nidhamu ya CAF ilitoa maamuzi ya kugawa lawama kwa pande zote mbili ambapo upande wa Senegal ulipata pigo baada ya kocha wao mkuu, Pape Bouna Thiaw, kufungiwa mechi tano za mashindano rasmi ya CAF huku wachezaji Cheikh Barou Ndiaye na Ismaïla Sarr wakifungiwa mechi mbili kila mmoja. Aidha, Senegal imetozwa faini ya dola 615,000.
Kwa upande wa Morocco, CAF imemfungia beki Achraf Hakimi mechi mbili na kiungo Ismaël Saibari mechi tatu, huku shirikisho likiamriwa kulipa faini ya dola 300,000. Pamoja na adhabu hizo, kamati hiyo pia imetupilia mbali malalamiko ya awali ya Morocco dhidi ya Senegal kuhusu ukiukwaji wa kanuni za mashindano kupitia vifungu vya 82 na 84. Morocco sasa inasubiri hatua zaidi za kisheria baada ya kuwasilisha pingamizi hilo dhidi ya maamuzi hayo ya mamlaka ya soka barani Afrika.

Post a Comment