BAKARI SHIME AWEKA HADHARANI KIKOSI CHA TWIGA STARS KUELEKEA WAFCON 2026
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya soka ya wanawake Twiga Stars, Bakari Shime ametangaza kikosi cha awali chenye jumla ya wachezaji 30 kitakachoanza kujiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake maarufu kama WAFCON.
Michuano hiyo imepangwa kuanza kurindima nchini Afrika Kusini kuanzia tarehe 17 Machi hadi tarehe 3 Aprili mwaka 2026 ambapo Tanzania imepangwa katika Kundi B pamoja na wenyeji Afrika Kusini, Ivory Coast na Burkina Faso.
Katika kikosi hicho kocha Shime amewajumuisha walinda mlango na mabeki ambao ni Najiat Abbas, Lidya Maximilian, Anastazia Katunzi, Christer Bahera, Donisia Minja, Ester Maseke, Winfrida Gerald na Janeth Christopher.
Safu hiyo inaendelea na wachezaji Stumai Abdallah, Joyce Lema, Elizabeth Chenge na Jamila Rajabu kutoka JKT Queens wakati Asha Mrisho anawakilisha Mashujaa Queens huku Nusrat Jafar akitokea Fountain Gate na Husna Mtunda akitokea Alliance Girls. Wachezaji wengine wa ndani walioitwa ni Diana Mnaly Maimuna Kaimu na Neema Shau kutoka Yanga Princess pamoja na Asha Omary na Aisha Juma kutoka Simba Queens.
Kikosi hicho kimeimarishwa zaidi na wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi akiwemo Enekia Kasonga na Julietha Singano wanaocheza nchini Mexico pamoja na Noela Luhala anayekipiga Lithuania. Safu ya ushambuliaji inaongozwa na nyota Vaileth Nicholaus, Suzan Adam na Hasnath Ubamba wanaocheza Misri akishirikiana na Opah Clement wa Hispania Clara Luvanga wa Saudi Arabia, Aisha Masaka wa England pamoja na Diana Lucas anayecheza nchini Uturuki.
Kocha Shime amesema lengo lake ni kuhakikisha Twiga Stars inafika hatua ya nusu fainali ili kujihakikishia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia kwani timu nne za juu ndizo zitakazopata fursa hiyo. Licha ya kukiri kuwa na kibarua kigumu cha kuwakusanya wachezaji wengi wanaocheza nje ya nchi kwa muda mrefu bado ana imani kubwa na kikosi chake. Hii itakuwa ni mara ya tatu kwa Twiga Stars kushiriki michuano hiyo baada ya kufanya hivyo mwaka 2010 na mwaka 2024 ambapo katika mara zote hizo timu iliishia hatua ya makundi.

Post a Comment