WADAU 1,200 KUKUTANA ARUSHA KUANDIKA HISTORIA MPYA KINGA YA JAMII
WADAU 1,200 wa sekta ya kinga ya jamii kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar watakutana katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha AICC kwa ajili ya mkutano mkubwa wa kihistoria katika kuelekea mapinduzi ya huduma za kijamii nchini.
Katika Mkutano huo ambao ni hatua kubwa katika kuimarisha ustawi wa wananchi, pia utashuhudia Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya mwaka 2023 ikizinduliwa rasmi.
Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya mwaka 2023 ndiyo dira kuu inayoelekeza namna ya kuimarisha mifumo ya usalama wa kipato na huduma za kijamii kwa kila Mtanzania chini ya kauli mbiu isemayo Kinga ya Jamii kwa Wote Msingi wa Maendeleo
Tukio hili la kihistoria litafanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) tarehe 09 Februari 2026.
Mkutano huu ambao umeratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira na Mahusiano kwa ushirikiano na mifuko ya NSSF PSSSF na WCF unalenga kujadili maendeleo na fursa lukuki zinazopatikana katika sekta ya kinga ya jamii huku ukikutanisha viongozi wa ngazi za juu wa serikali, wataalamu wa sera na wadau wa ustawi wa jamii ili kuweka mikakati ya pamoja ya kumlinda mwananchi.
Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira na Mahusiano, Revocatus Kasimba amebainisha kuwa maandalizi ya mkutano huo mkubwa yapo katika ngazi za juu na kusisitiza kuwa uwepo wa viongozi waandamizi wa serikali unadhihirisha umuhimu wa mazungumzo haya katika kuimarisha utu na usalama wa maisha ya wananchi wote.
"Wananchi na wadau wote wanahimizwa kufuatilia tukio hili muhimu ambalo linaweka msingi mpya wa jinsi Tanzania inavyojali na kulinda utu na maisha ya watu wake kupitia mifumo imara na endelevu ya kinga ya jamii" anasema Kasimba.
Uzinduzi wa sera hii ndani ya mkutano wa wadau ni hatua ya kimkakati inayolenga kuhakikisha kuwa kile kinachopangwa na serikali kinapata baraka na uelewa wa pamoja kutoka kwa watekelezaji na wanufaika ili kuleta matokeo ya haraka katika ustawi wa jamii nchini kote.

Post a Comment