ZIARA YA WAZIRI WANG YI: NEEMA YA AJIRA 82,000 NA BIASHARA YA DOLA BILIONI 5.2 ZATAJWA
Uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China umezidi kuimarika ambapo takwimu za biashara na uwekezaji zinaonyesha mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali.
Hadi kufikia mwaka 2024, thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia takriban dola za Marekani bilioni 5.2, huku kampuni za China zikiendelea kuwekeza kwa kasi katika sekta za viwanda, kilimo, huduma, usafirishaji, mawasiliano na utalii.
Katika kielelezo kingine cha ukuaji huo, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imesajili miradi 343 ya China yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.1 kwa mwaka 2025 pekee. Uwekezaji huo umekuwa na tija kubwa kwa jamii kwa kuzalisha jumla ya ajira 82,404 kwa Watanzania.
Huku ushirikiano wa mataifa hayo mawili yakizidi kuimarika, Mjumbe wa Kamati ya Kisiasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Wang Yi, anatarajiwa kuwasili nchini kesho kwa ziara ya siku mbili ya kiserikali.
Akiwa nchini, Mhe. Wang Yi atapokelewa na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.). Vilevile, kiongozi huyo anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ziara hii inalenga kufuatilia na kuanza utekelezaji wa makubaliano yaliyopitishwa wakati wa mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika Beijing mnamo Septemba 2024. Aidha, ziara hiyo ni muendelezo wa kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na kihistoria uliodumu kwa miongo sita sasa.
Mbali na biashara, nchi hizi mbili zimeendelea kushirikiana katika miundombinu ya uchukuzi, ambapo reli ya TAZARA yenye urefu wa kilomita 1,860 imebaki kuwa alama ya urafiki na mshikamano. Msingi wa ushirikiano huu uliwekwa na waasisi wa mataifa haya, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong, na unaendelea kuenziwa kwa vitendo na viongozi wa sasa.

Post a Comment