VIPIGO AFCON VYALETA KIZAAZAA GABON

 


.Benchi la ufundi lavunjwa nahodha Ubameyang marufuku kuchezea Gabon

Serikali ya Gabon imechukua maamuzi mazito kwa kumpiga marufuku nahodha na mshambuliaji wao tegemeo, Pierre-Emerick Aubameyang, kutoichezea tena timu ya taifa, huku ikisimamisha shughuli zote za timu hiyo kwa muda usiojulikana baada ya kufanya vibaya katika michuano ya AFCON 2025 nchini Morocco.
Gabon, maarufu kama ‘The Panthers’, wamefungashiwa virago katika hatua ya makundi baada ya kupoteza michezo yote mitatu ya Kundi F, matokeo ambayo yameleta simanzi na hasira nchini mwao.
Licha ya kupewa nafasi ya kufanya vizuri (dark horses), Gabon ilianza kwa kupoteza 1-0 dhidi ya Cameroon, kabla ya kukumbana na kipigo cha kushtua cha 3-2 kutoka kwa Msumbiji. Katika mchezo wao wa mwisho uliopigwa Jumatano jioni, walikubali kichapo kingine cha 3-2 kutoka kwa mabingwa watetezi, Ivory Coast, ambao walifunga mabao mawili ya ushindi dakika za mwisho.
Kufuatia matokeo hayo, serikali imemfuta kazi kocha mkuu, Thierry Mouyouma, na kuisimamisha timu nzima ikitaka majibu ya kile kilichosababisha aibu hiyo Kaskazini mwa Afrika.
"Kutokana na kiwango cha hovyo na cha kusononesha kilichoonyeshwa na 'The Panthers' kwenye AFCON, serikali imeamua kuvunja benchi la ufundi na kuisimamisha timu ya taifa hadi hapo itakapotangazwa tena," alisema Waziri wa Michezo nchini humo, Simplice-Désiré Mamboula.
Jambo la kushangaza zaidi ni uamuzi wa serikali kuwapiga marufuku wachezaji wawili wenye uzoefu mkubwa zaidi; Pierre-Emerick Aubameyang na nahodha Bruno Ecuele Manga. Aubameyang alifunga bao moja katika mchezo dhidi ya Msumbiji lakini hakucheza mechi ya mwisho dhidi ya Ivory Coast.
Kwa kuzingatia umri wao (Aubameyang miaka 36 na Manga miaka 37), wataalamu wa soka wanahisi huenda wachezaji hao wameishacheza mechi yao ya mwisho kwa taifa lao.
Hata hivyo, uamuzi huu wa serikali kuingilia masuala ya soka unatarajiwa kuleta madhara makubwa, kwani Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limekuwa na msimamo mkali dhidi ya serikali yoyote inayojihusisha na uendeshaji wa soka, jambo linaloweza kupelekea Gabon kufungiwa uanachama.

No comments