MWANARIADHA SISILIA PANGA ANG’ARA BRAZIL, ATWAA DHAHABU



Mwanariadha nyota wa Tanzania, Sisilia Panga, amehitimisha mwaka 2025 kwa kishindo baada ya kunyakua medali ya dhahabu katika mbio maarufu za barabarani za Sao Silvestre Road zilizofanyika Desemba 31 jijini Sao Paulo, nchini Brazil.

Katika ushindi huo wa kihistoria, Sisilia alitumia dakika 51 na sekunde 08, akiwagaragaza wanariadha mashuhuri duniani na kuonesha uvumilivu wa hali ya juu pamoja na mbinu za kipekee zilizomuweka kileleni mwa ushindani huo mkubwa.

Mafanikio haya ya Sisilia Panga yamezidi kuimarisha hadhi ya Tanzania katika ramani ya riadha kimataifa, ikithibitisha kuwa ni chimbuko la wakimbiaji wa mbio ndefu wa daraja la kwanza.

Akizungumzia mafanikio hayo, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogath Stephen, alimpongeza Sisilia kwa nidhamu ya hali ya juu na kujituma kulikopelekea ushindi huo mnono. Alieleza kuwa mafanikio hayo ni mfano wa kuigwa kwa wanariadha wengine wanaochipukia nchini.

Rais huyo wa RT alitumia fursa hiyo kuwataka wanariadha nchini kuongeza bidii katika mazoezi na kudumisha nidhamu binafsi, akisisitiza kuwa uzalendo na fahari ya kulilinda jina la taifa ni nyenzo kuu za mafanikio kimataifa.

Ushindi wa Sisilia Panga nchini Brazil unakuja kama medali nyingine ya dhahabu ya kihistoria kwa taifa ndani ya mwaka 2025. Mafanikio hayo yanafuatia hatua nyingine kubwa iliyofikiwa na Alphonce Simbu, ambaye aliandika historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu ya dunia katika mbio za Marathon jijini Tokyo, Japan.

No comments