DKT. KIKWETE AHIMIZA UBUNIFU WA FEDHA ZA AFYA KATIKA MKUTANO WA ECSA-HC NCHINI ESWATINI
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ametoa mwito mzito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) kuacha kutegemea ufadhili wa nje na badala yake kubuni vyanzo mbadala vya mapato ili kugharamia miradi ya afya.
Akizungumza Februari 2 hadi 3, 2026, katika Mkutano wa 67 wa Mawaziri wa Afya uliofanyika Ezulwini nchini Eswatini, Dkt. Kikwete amesisitiza kuwa mabadiliko ya kiuchumi duniani yamesababisha kupungua kwa wafadhili, jambo linalohitaji suluhisho la kudumu kutoka ndani ya bara la Afrika ili kulinda usalama wa afya kwa wananchi.
Katika hotuba yake, Dkt. Kikwete amewakumbusha watunga sera kuwa serikali haina uhalali wa kuwaambia wananchi kuwa huduma za afya zinasitishwa kwa sababu wafadhili wameacha kutoa fedha. Alieleza kuwa ni jukumu la viongozi kuumiza vichwa na kutafuta mbinu mpya za kifedha ili kuhakikisha miradi iliyokwishaanzishwa haifi.
Kama suluhisho la kikanda, alipendekeza nchi hizo kuimarisha mfumo wa manunuzi ya pamoja ya dawa na vifaa tiba kwa bei nafuu, mkakati utakaosaidia kupunguza gharama na kuongeza uhimilivu wa mifumo ya afya katika nchi wanachama.
Vilevile, Dkt. Kikwete alitumia fursa hiyo kuelezea mafanikio makubwa ambayo Tanzania imeyapata chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Alibainisha kuwa Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa barani Afrika baada ya kufanikiwa kushusha kiwango cha vifo vya akina mama wajawazito kutoka vifo 560 hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai laki moja.
Mafanikio haya yanaifanya Tanzania kuwa njiani kutimiza lengo la Umoja wa Mataifa la SDG 3.1 linalotaka vifo hivyo kupungua hadi kufikia 70 ifikapo mwaka 2030, jambo linalotokana na ushirikiano imara kati ya serikali na wadau kama taasisi ya JMKF.
Akigusia utendaji wa taasisi yake, alieleza jinsi mradi wa Jamii Salama unavyosaidia maeneo ya pembezoni mkoani Tabora, hususan katika wilaya za Uyui na Sikonge.
Kupitia kliniki zinazotembea, mradi huo umeweza kuwafikia zaidi ya akina mama 1,500 kwa huduma za ultrasound na tiba ya malaria, huku watoto wa shule zaidi ya 3,200 wakifikiwa na elimu ya afya.
Mwishoni mwa mkutano huo, Dkt. Kikwete aliongoza ujumbe wa mawaziri kuonana na Mfalme Mswati III wa Eswatini, ambaye aliahidi kufikisha ripoti ya majadiliano hayo kwa viongozi wakuu wa nchi wanachama ili kuongeza msukumo wa kisiasa katika kuimarisha sekta ya afya.
Post a Comment