SENEGAL, MOROCCO ZALIMWA FAINI KWA KULETA ZA KULETA FAINALI AFCON



Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) limeamua kuingia uwanjani na kadi nyekundu ya faini inayozidi dola za kimarekani milioni moja kufuatia "vurugu mechi" zilizotokea kwenye fainali ya kibabe ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). Hii siyo faini tu, bali ni kama mpira uliogonga mwamba kisha ukarudi uwanjani, maana makocha na mastaa kadhaa wamepigwa "pini" ya kutocheza michezo ijayo.

Baada ya siku kumi za vuta n'kuvute tangu fainali hiyo iliyozua mijadala kuliko VAR yenyewe kumalizika, CAF imetoa tamko rasmi Jumatano hii ikisema Senegal watalazimika kukohoa dola 615000  kwa utovu wa nidhamu. Kocha wao, Pape Thiaw, amepigwa 'benchi' michezo mitano kati ya sita ya kufuzu AFCON 2027, huku akipigwa faini ya 'penati' ya dola laki moja kwa kuichafua taswira ya soka la Afrika.

Mchezo huo ulikuwa na kadha wa kadhaa, pale Senegal walipoamua 'kugoma' na kutoka nje kupinga uamuzi wa mwamuzi kuipa Morocco penati baada ya kurejea kwenye VAR. Papo hapo mashabiki walitaka kuvamia uwanja kama washambuliaji wanavyovamia lango, na waandishi wa habari nao wakaanza kuzichapa kavukavu. 

Ingawa Morocco walikosa penati hiyo baada ya mchezo kusimama kwa dakika 15, Senegal walikuja juu na kuchukua ubingwa kwenye dakika za nyongeza, lakini kocha wa Morocco, Walid Regragui, amesema tukio hilo limeleta "shame" ( aibu )kubwa uwanjani.

Nao Morocco hawajabaki salama; wamepigwa faini ya dola 315,000 kwa tabia mbovu za wachezaji na washabiki wao. Balaa kubwa zaidi limetajwa kuwa ni watoto wa kuokota mipira (ball boys) ambao walijaribu 'kuiba' taulo la golikipa wa Senegal, Edouard Mendy, ili kumtoa mchezoni. 



Pia wamepigwa faini ya dola laki moja kwa kuivamia sehemu ya VAR na kumzuia mwamuzi Jean-Jacques Ndala kufanya kazi yake, huku washabiki wao wakipigwa faini ya dola 15,000 kwa kutumia 'leza' kuwapumbaza wachezaji wa Senegal.

Mwisho wa siku, CAF imetupa kule ombi la Morocco la kutaka matokeo yabatilishwe na wao wapewe ubingwa wa mezani. Wakati timu zote zikijiandaa kwa ajili ya Kombe la Dunia 2026 kule Marekani, Mexico, na Canada, Morocco itabidi ijipange upya maana itakutana na miamba ya soka kama Brazil, huku Senegal ikipangwa Kundi I kukabiliana na wababe wa Ulaya, Ufaransa.

No comments