JUMA JUX AN’GARA NIGERIA: ASHINDA TUZO YA MSANII BORA WA KIUME AFRIKA MASHARIKI (AFRIMMA)
Msanii wa Bongo Fleva, Juma Makambala, maarufu kama Juma Jux, ameiandikia Tanzania historia mpya baada ya kushinda tuzo ya Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki katika tuzo za African Music Magazine Awards (AFRIMMA) zilizofanyika jijini Lagos.
Jux amefanikiwa kuibuka mshindi katika kipengele hicho kilichokuwa na ushindani mkali, akiwashinda mastaa wenzake kutoka Tanzania kama Diamond Platnumz, Marioo, na Mbosso. Aidha, amewapiku wasanii wengine wakubwa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki wakiwemo Bien (Kenya), Bruce Melodie na Element Elee’h (Rwanda), Joshua Baraka (Uganda), Sat-B (Burundi), pamoja na Yared Negu (Ethiopia).
Mafanikio na Shukurani
Ushindi huu umekuja wakati mwafaka kwa Jux, ambaye hivi karibuni amekuwa akifanya vizuri nchini Nigeria, ikiwemo kufanya shoo kubwa jijini Lagos iliyovutia mashabiki wengi. Tuzo hii ni uthibitisho wa kukua kwa chapa yake na ubora wa muziki wa Bongo Fleva unaozidi kuvuka mipaka.
Katika hotuba yake ya ushindi, Jux alimshukuru Mungu, familia, na mashabiki wake duniani kote. Kwa namna ya kipekee, alitangaza kuitoa tuzo hiyo kwa mwanawe, Rakim.
Pongezi kutoka BASATA
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) halikubaki nyuma, ambapo limempongeza Juma Jux kwa mafanikio hayo makubwa. BASATA imeeleza kuwa ushindi wa Jux ni heshima kwa taifa kwani ameiwakilisha na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika jukwaa la kimataifa la muziki barani Afrika.

Post a Comment