Viongozi wa Kiislamu wamuunga mkono Rais Samia, Wasisitiza Maridhiano na Haki
Viongozi wa Taasisi 22 za Kiislamu
nchini Tanzania, wakiongozwa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakar
Zubeir bin Ally, wametoa tamko kali la kulaani vurugu zilizotokea baada ya
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Pamoja na tamko hilo wameeleza bayana
kuwa wanaunga mkono kikamilifu hatua za serikali za kurejesha utulivu na
kuanzisha maridhiano ya kitaifa.
Tamko hilo lilitolewa baada ya viongozi
hao kumaliza ibada maalum ya Itikafu iliyofanyika katika Msikiti wa
Mfalme Mohammed wa Sita, Makao Makuu ya BAKWATA.
Madhumuni ya Itikafu hiyo ilikuwa ni
kumkimbilia Mwenyezi Mungu, kutoa dua kwa waliofariki na walioathirika, na
kutafakari njia sahihi ya kuipeleka nchi mbele baada ya matukio mazito ya
uchomaji nyumba, vituo vya mafuta, uharibifu wa miundombinu, na kusababisha
vifo vya raia na askari.
Viongozi hao wamesisitiza kwamba
wamehuzunishwa sana na hali iliyotokea, ikiathiri taswira ya nchi, na wamelaani
matamko yaliyotolewa na baadhi ya watu au vikundi yenye kuchochea hasira na
kuharibu amani.
Maazimio Makuu Yaliyotangazwa:
- Kuunga Mkono Rais Samia: Taasisi hizo zimepokea kwa
heshima na kuunga mkono Hotuba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa
bungeni mnamo Novemba 14, 2025.
- Tume Huru na Maridhiano: Wameunga mkono hatua ya Rais ya
kuunda Tume Huru ya Uchunguzi (Enquiry Commission) kubaini kiini
cha tatizo, ambayo taarifa yake itatumika kuongoza mazungumzo ya
maridhiano ya kitaifa.
- Maridhiano Siyo Kichaka cha Uhalifu: Ingawa wanaunga mkono maridhiano,
wameonya kuwa mchakato huo usitumike kuficha uhalifu. Wamesisitiza umuhimu
wa kufanya uchunguzi wa kina, usio na upendeleo, kubaini waliochochea,
kupanga, na kuratibu uhalifu huo ili haki isimame sawa.
- Wito kwa Vijana na Watanzania: Taasisi za Kiislamu zimewataka
Waislamu na Watanzania wote kudai haki zao kwa kufuata sheria na taratibu
zilizowekwa, na wamekataa mijadala ya mitandaoni inayoeneza chuki za
kidini, kikabila, au kikanda. Wamefika mbali kwa kuwasihi vijana kuitumia
tarehe 9 Desemba kukaa nyumbani na wazazi wao kwa ajili ya kuombea taifa
na kuepuka mikusanyiko inayoweza kusababisha vurugu.
Taasisi hizo pia zimeahidi kuwa daraja
la kuunganisha Watanzania na zimeitaka Serikali iwaangalie kwa jicho la
huruma waliofiwa na walioharibikiwa na mali zao. Mufti ametoa wito kwa Waislamu
kutumia kauli za kujenga na kuleta umoja.

Post a Comment