RAIS SAMIA AZINDUA TUME YA UCHUNGUZI WA VURUGU ZA UCHAGUZI, AIPIGIA MSTARI FEDHA ZA WAANDAMANAJI, NGO

 


Rais Samia Suluhu Hassan amezindua Tume ya Uchunguzi wa vurugu zilizotokea siku ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, huku akiitaka kuchunguza chanzo cha fedha wanazodaiwa kupewa vijana walioandamana.

Rais Samia alisema hayo jana Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma wakati akiizindua na kuipa Tume miezi mitatu kukamilisha uchunguzi huo. Alisisitiza kuwa kilichotokea siku ya uchaguzi hakikutarajiwa kutokea nchini kutokana na historia ya amani na utulivu wa kisiasa.

“Hata kama tuna vipindi tulikuwa hatuna utulivu wa kisiasa lakini hatukufikia kiasi hiki kilichofikia. Tume itakabidhiwa hadidu za rejea watakazokwenda kuziangalia na kuzifanyia kazi,” alisema Rais Samia.

Hadidu za Rejea Muhimu za Tume

Rais Samia aliiagiza Tume kuangalia na kuchunguza mambo mbalimbali, ikiwemo kiini cha vurugu na matamshi ya vyama vya siasa. Hadidu kuu za rejea ni:

  • Kiini cha Tatizo: Kuchunguza sababu hasa zilizosababisha vijana kuingia barabarani na kufanya vurugu.

  • Madai ya Haki: Kubaini ni haki gani hasa vijana wanazodai ili Serikali iweze kuzifanyia kazi kwa haraka na kuzipata.

  • Fedha na NGO: Kuchunguza chanzo cha fedha walizolipwa vijana waandamanaji na kuangalia ushiriki (role) wa Taasisi Zisizo za Serikali (NGO) za ndani na nje ya nchi katika vurugu hizo.

  • Matamshi ya Upinzani: Kuangalia matamshi ya vyama vya upinzani vilivyoahidi kuzuia uchaguzi na kubaini kiini cha kauli hizo. Tume pia iangalie uhusiano wa vyama hivyo na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Msajili wa Vyama.

  • Mbinu za Kukabiliana: Kuangalia njia zilizochukuliwa kukabiliana na vurugu zilizotokea, kwa kuzingatia kuwa Tume ina wajumbe wastaafu wa jeshi na polisi.

Rais Samia alieleza kuwa lengo la kuunda Tume hii ni kukusanya mapendekezo ambayo yatatumika kama ajenda kwenye Tume ya Maridhiano iliyoahidiwa awali, akisisitiza kuwa uundaji wa Tume hiyo umeendana na Sheria ya Tume za Uchunguzi ya Mwaka 2023.

No comments