MOROCCO NJE, GAMONDI NDANI
Na Rahel Pallangyo
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesitisha mkataba na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Ali Suleiman 'Morocco'.
Taarifa ya TFF imemtangaza Kocha Miguel Gamondi, raia wa Argentina, kuwa Kaimu Kocha Mkuu, akichukua jukumu la kuiongoza timu hiyo kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika nchini Morocco Desemba mwaka huu.
Gamondi, ambaye mara nyingi hupenda falsafa ya soka la kumiliki mpira, atatakiwa kufanya uamuzi mgumu: Je, aanzishe falsafa yake au aendeleze ulinzi imara na mbinu za ‘transitions’ alizoacha Morocco? Kila jaribio la kuanzisha kitu kipya linaweza kugharimu utendaji na utulivu wa timu.
Taifa Stars kwenye fainali hizo ipo Kundi C na vigogo kama Nigeria na Tunisia pamoja na jirani Uganda.
Gamondi anahitaji kufanya kazi ya ziada na ya haraka ili kuijenga timu na kuhakikisha wachezaji wanampokea na kuamini mbinu zake kwa haraka.
Morocco amekuwa kwenye benchi la Taifa Stars mara tatu na kuiwezesha Taifa Stars kufuzu fainali za mataifa ya Afrika mfululizo kuanzia 2019 na amekuwa na mafanikio.


Post a Comment