DAVID BECKHAM SASA NI SIR ,ATUNUKIWA HESHIMA NA MFALME WA UINGEREZA




MMLIKI wa klabu ya Ligi Daraja la Pili ya Salford City ambaye pia ni mmiliki mwenza wa timu ya MLS ya Inter Miami , David Beckham sasa jina lake linaanza na Sir.

Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, ametunukiwa rasmi cheo hicho cha heshima  chenye hadhi kubwa nchini Uingereza kutokana na utumishi wake kwa taifa hilo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 50, ambaye jina lake lilitajwa kwenye orodha ya Tuzo za Siku ya Kuzaliwa ya Mfalme Charles mapema mwaka huu, alikabidhiwa heshima hiyo na Mfalme Charles mwenyewe katika sherehe iliyofanyika Berkshire, Jumanne.

"Siwezi kujisikia fahari zaidi," alisema Beckham baada ya sherehe. "Watu wanajua jinsi ninavyopenda nchi yangu... nimekuwa nikisema kila marakwa familia yangu umuhimu wa Ufalme."

Beckham aliongeza kuwa ameridhika na namna ambavyo ufalme wa Uingereza unavyopendwa na kuheshimiwa kote ulimwenguni: "Nina bahati ya kusafiri kote ulimwenguni na watu wote wanataka kuzungumza nami kuhusu ufalme wetu. Hilo linanipa fahari."

Akiwa katika Kasri la Windsor, Beckham aliambatana na mkewe, Victoria Beckham, ambaye alipokea tuzo ya OBE mwaka 2017 kwa huduma zake kwenye tasnia ya mitindo, pamoja na wazazi wake, Sandra na David.



Urithi wa Beckham: Zaidi ya Uwanja

Soka: Beckham aliichezea nchi yake mara 115 na kuiongoza timu ya 'Three Lions' kama nahodha kwa miaka sita, kuanzia 2000 hadi 2006. Alicheza kwenye Kombe la Dunia mara tatu na Kombe la Mataifa ya Ulaya (Euro) mbili. Katika ngazi ya klabu, alichezea timu kubwa kama Manchester United, Real Madrid, LA Galaxy, AC Milan, na Paris St-Germain.

Huduma kwa Jamii: Mbali na mchango wake uwanjani, Beckham alishirikiana na shirika la msaada la kibinadamu la Unicef tangu 2005 na pia alikuwa na jukumu muhimu katika kufanikisha London kupata fursa ya kuandaa Michezo ya Olimpiki ya 2012.

Heshima za Awali: Beckham alipewa tuzo ya OBE na Malkia Elizabeth II mwaka 2003. Pia, alisimama kwenye foleni kwa zaidi ya saa 12 ili kutoa heshima zake za mwisho kwa Malkia aliyelala katika hali ya heshima baada ya kifo chake mwaka 2022.

Ubalozi: Mwaka 2024, aliteuliwa kuwa balozi wa King's Foundation, akisaidia programu za elimu za Mfalme Charles na juhudi za kuhakikisha vijana wanaelewa zaidi kuhusu asili.

No comments