BMT Yakabidhi Bendera Timu Tatu Kuelekea Afrika Kusini na Angola



Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limethibitisha dhamira yake ya kusimamia, kukuza, na kuendeleza michezo yote nchini kwa kukabidhi bendera ya Taifa kwa jumla ya timu tatu tofauti zinazoelekea kushiriki mashindano makubwa ya kimataifa.

Mchakato wa kukabidhi bendera ulianza  Desemba 3, 2025, ambapo timu ya taifa ya mchezo wa kutunisha misuli (Bodybuilding) ilikabidhiwa bendera na BMT. Timu hiyo inatarajiwa kushiriki Mashindano ya Dunia yatakayoanza Desemba Sita 2025 nchini Afrika Kusini, yakihusisha zaidi ya mataifa kumi. 

Akikabidhi bendera katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Afisa Michezo Mwandamizi wa BMT, Charles Maguzu, alisisitiza kuwa Baraza litaendelea kusimamia michezo yote kama sehemu ya kuinua sekta hiyo na kuitangaza Tanzania kimataifa. 

Alitoa wito kwa wadau wa michezo kuungana na BMT katika kuipa nguvu michezo hiyo, huku akifafanua kwamba Tanzania itawakilishwa na wachezaji watatu ambao ni Martha Mabula, Noah Schembe, na Obadia Mwampeta.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Nahodha wa timu, Martha Mabula, alieleza kuwa maandalizi makini waliyofanya yanawapa imani ya kufanya vizuri na kulinda heshima ya Taifa. "Binafsi nimejipanga vizuri katika kipengele cha wanawake. Maandalizi yote yamekamilika na tunashukuru BMT kwa kutusimamia kwa hali na mali. Tumejipanga kupambana na kufanya vizuri,” alisema Mabula, akionesha utayari wa timu yake.



Siku mbili baadaye,  Desemba 5 , 2025, timu za taifa za mchezo wa kuogelea na mpira wa meza nazo zilikabidhiwa bendera kuelekea Angola. Timu hizo zinatarajiwa kushiriki Mashindano ya Nne ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, yatakayofanyika kuanzia Desemba 10 hadi 20. 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Ofisa Michezo Mwandamizi wa BMT, Charles Maguzu, aliwataka wachezaji hao kuhakikisha wanapigania bendera ya Taifa kwa nguvu zote. Maguzu alifafanua kuwa Serikali imetoa fedha na mavazi kwa ajili ya safari na maandalizi yao, huku akiwaombea warejee na makombe na medali.

Kwa upande wa uongozi wa safari, Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau, alieleza kuwa msafara huo utahusisha jumla ya watu saba: wachezaji watatu, viongozi wawili na makocha wawili. 

Tandau alibainisha kwamba Tanzania itawakilishwa na wachezaji wawili katika timu ya kuogelea, na mchezaji mmoja katika timu ya mpira wa meza. Naye Meneja wa timu hizo, Halima Bushiri, ambaye pia ni Afisa Michezo wa BMT, alihitimisha kwa kusema kuwa maandalizi yamekamilika kikamilifu na timu zote zinajipanga kurejea na ushindi mkubwa.

No comments