Polisi yahamasisha umma kukataa vurugu
Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa wito kwa wananchi wote kwa nafasi zote kuanzia ngazi ya familia kuwakataa watu wanaohamasisha uvunjifu wa amani na sheria kwani malengo yao ni kuharibu Taifa na kuwarudisha watanzania kwenye machungu ya Oktoba 29, 2025.
Aidha limesema kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na usalama linaendelea kufuatilia kwa karibu yanayoendelea kwenye Mitandao ya Kijamii na kwenye makundi sogozi .
Polisi pia imeeleza katika taarifa yake kwa Vyombo vya habari kuwa linaendelea kuzuia uhalifu sambamba na kuwakamata wale wanaofanya makosa mbalimbali ikiwemo ya Kimtandao kwa wale wanaoendesha makundi mbalimbali katika Mitandao ya kijamii ya kuhamasisha uhalifu na kuwachukulia hatua kulingana na sheria za nchi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime katika taarifa hiyo amelaani pia kile kinachoelezwa katika makundi hayo ya mitandao ya Kijamii ikiwemo ya wito wa kutoshika silaha katika maandamano hayo ikiwa mwandamanaji hakupitia mafunzo na badala yake waachie silaha wenye mafunzo.
"Kupitia Mitandao na Klabu mbalimbali za Mtandaoni wanahamasishana pia kusiwe na shughuli nyingine itakayoendelea katika jamii. Pia wahakikishe wanaharibu na kuchoma moto minara yote ya mawasiliano ili nchi nzima ikose mawasiliano, wanahamasishana pia wahakikishe bandari ya Dar Es Salaam haifanyi kazi kwani watafunga barabara zote zinazoingia na kutoka Bandarini na zile zinazoiunganisha Tanzania na nchi za jirani." Amesema Misime.
Aidha waandamanaji hao pia wanahamasishana kuwafuata popote walipo watumishi wa serikali ili kuwadhuru.

Post a Comment