SITA WAPITISHWA KUWANIA KITI CHA SPIKA



Zoezi la uteuzi wa wagombea wa uchaguzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekamilika leo saa 10:00 Alasiri, huku wagombea sita  kutoka vyama sita  vya siasa wakithibitishwa na Katibu wa Bunge na Msimamizi wa Uchaguzi,  Baraka I. Leonard.

Uchaguzi huu unafanywa kwa mujibu wa Ibara ya 86(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, pamoja na Kanuni ya 9 na Nyongeza ya Kwanza ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2025.

Katibu wa Bunge alikamilisha zoezi la uteuzi baada ya kutoa Tangazo namba 14824A mnamo tarehe 4 Novemba, 2025, akivitaka vyama vya siasa kuwasilisha majina ya wagombea wao kabla ya saa 10:00 jioni ya tarehe 10 Novemba, 2025.

Orodha ya Wagombea 

Hadi kufikia saa 10:00 Alasiri leo, wagombea waliowasilishwa na vyama vyao na ambao wameidhinishwa ni sita, nao ni:  Mussa Azzan Zungu kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM); Veronica Charles Tyeah kutoka Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA); Anitha Alfan Mgaya kutoka Chama cha National League for Democracy (NLD);  Chrisant Nyakitita kutoka Chama cha Democratic Party (DP); Ndonge Said Ndonge kutoka Chama cha Alliance for Africa Farms Party (AAFP); na  Amin Alfred Yango kutoka Chama cha Aliance for Democratic Change (ADC).

Akitoa ufafanuzi, Katibu wa Bunge, Baraka I. Leonard, amesema kuwa baada ya uchambuzi wa kina uliozingatia nafasi ya Kiti cha Spika, sifa za wagombea na matakwa mengine ya Kisheria na Kikanuni, ameridhika kwamba Wagombea wote wametimiza masharti ya Kanuni za Uchaguzi.

Uchaguzi kufanyika Kesho

Kwa mujibu wa utaratibu uliotolewa, Katibu wa Bunge atawasilisha majina ya wagombea hao sita kwa Wapiga kura, ambao ni Wabunge Wateule wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili Uchaguzi ufanyike.

No comments