WAPUUZENI WANAOSAMBAZA TAARIFA ZA UHAMIAJI KUPOKA PASIPOTI
Idara ya Uhamiaji imetoa taarifa hadharani ikikanusha vikali taarifa zinazosambazwa kwa njia ya sauti (Audio Clip) kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa raia wa Tanzania waliopo nje ya nchi wanaporejea nchini kupitia viwanja vya ndege au vituo vingine vya kuingia nchini wananyang'anywa pasipoti na fedha zao.
Aidha clip hiyo inadai kuwa baada ya kupokonywa hati hizo wanatakiwa kwenda kufanyiwa mahojiano Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dodoma.
Katika taarifa yake, Idara ya Uhamiaji imesisitiza kuwa taarifa hizo "ni za uzushi wenye lengo la kupotosha umma na kuleta taharuki kwa jamii."
Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Makao Makuu, Dodoma, ambaye alitoa taarifa hiyo, amewataka Watanzania wote kuzipuuza taarifa hizo za uzushi.
Taarifa hiyo pia imesisitiza umuhimu wa wananchi kutegemea taarifa rasmi kutoka vyanzo vinavyotambulika vya Serikali.

Post a Comment