DKT MAPANA ACHOMOLEWA BASATA APELEKWA KUWA NAIBU KATIBU MKUU VIJANA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa watendaji wawili kuhudumu  katika Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana. 

Kwa mujibu wa Taarifa kwa Vyombo vya Habari iliyotolewa Dar es Salaam na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ikikariri taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, viongozi walioteuliwa ni Bi. Jenifa Christian Omolo kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana na Dkt. Kedmon Elisha Mapana ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu. 

Kabla ya uteuzi huo, Bi. Omolo alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha wakati Dkt. Mapana alikuwa Katibu Mtendaji, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Aidha, Kurugenzi ya Mwasiliano ya Rais Ikulu imetangaza kuwa uapisho wa viongozi walioteuliwa utafanyika Ikulu Chamwino, Dodoma, tarehe 21 Novemba, 2025 saa 8.00 mchana.

UCHAMBUZI

Uteuzi huu unaonekana kama hatua yenye maono mapana, ikileta mchanganyiko wa uzoefu wa Utawala na Fedha pamoja na uzoefu wa karibu wa Vijana na Burudani.

Usimamizi wa Rasilimali Fedha: 

Uteuzi wa Bi. Jenifa Christian Omolo kama Katibu Mkuu una maana kubwa. Kuja kwake kutoka Wizara ya Fedha kunaashiria umuhimu wa Serikali wa kuweka nidhamu ya kifedha na usimamizi bora wa rasilimali katika ofisi inayoshughulikia miradi na mipango mingi ya vijana. Uzoefu wake wa utawala wa fedha unatarajiwa kuongeza ufanisi wa matumizi ya bajeti za maendeleo ya vijana.

 Uteuzi wa Dkt. Kedmon Elisha Mapana kama Naibu Katibu Mkuu umepokelewa kwa msisimko mkubwa kwani  Dkt. Mapana, kupitia BASATA, alikuwa kiungo cha moja kwa moja na kundi la vijana, akisimamia sekta inayotoa ajira kwa vijana wengi kupitia muziki, filamu, na sanaa. Uzoefu wake katika:

Kutambua Vipaji: 

Dkt. Mapana anajua jinsi ya kutambua uwezo na vipaji vilivyofichika vya vijana, akipambana na changamoto zao za kisaikolojia na kijamii.Pia anajua lugha ya vijana na jinsi ya kuwasiliana nao kuhusu fursa za Serikali, huku akitumia majukwaa ya sanaa kama njia ya kuwafikia.

Kuunganisha Sekta Rasmi na Isiyo Rasmi: 

Anatarajiwa kuleta uzoefu wa jinsi ya kuwafanya vijana wanaojishughulisha na kazi zisizo rasmi kuwa sehemu rasmi ya uchumi wa taifa.

Ushirikiano kati ya Katibu Mkuu mwenye asili ya Fedha (Bi. Omolo) na Naibu Katibu Mkuu mwenye asili ya Vijana/Sanaa (Dkt. Mapana) unaonekana kuwa kikosi kazi imara kilichopangwa kwa makusudi. Lengo kuu la Rais Samia linaonekana kuwa ni kuhakikisha Ofisi ya Vijana inakuwa na uongozi unaoweza kuleta pesa na utaratibu (Omolo) huku ikijua jinsi ya kuwafikia na kuwahamasisha vijana (Mapana).


No comments