MSHTUKO MZITO: MC Pilipili, MC wa Taifa, Afariki Dunia Ghafla Dodoma



Tasnia ya sanaa na burudani nchini Tanzania imeingia katika simanzi kubwa kufuatia kifo cha ghafla cha mchekeshaji na mshereheshaji maarufu, Emmanuel Mathias, anayejulikana kwa jina la jukwaani kama MC Pilipili.

MC Pilipili, ambaye alijipachika jina la utani la 'MC wa Taifa', amefariki dunia ghafla mchana wa leo, Novemba 16, 2025, jijini Dodoma, ambako alikuwa amesafiri kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ya ushereheshaji jioni. Kifo chake kimeacha mshtuko mkubwa kutokana na jinsi alivyokutwa na mauti ghafla akiwa katika safari ya kikazi.

Taarifa za msiba huu zimehakikishwa na mamlaka za Hospitali ya General, Dodoma.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Ernest Ibenzi, alithibitisha kuupokea mwili wa marehemu.

"Ni kweli tumepokea mwili wa mchekeshaji maarufu nchini MC Pilipili. Amefikishwa hapa hospitalini akiwa tayari amefariki dunia," alisema Dkt. Ibenzi.

MC Pilipili atakumbukwa kama mmoja wa washereheshaji mahiri na wa kipekee ambaye aliweka viwango vipya vya taaluma hiyo nchini.

Mafanikio yake yanaonekana wazi kupitia takwimu zake mwenyewe, ambapo alijinadi kuwa amesherehesha Harusi zaidi ya 3060 zenye furaha.

Mafanikio yake hayakuishia jukwaani tu. Alikuwa na ushawishi mkubwa mitandaoni, akionyesha jinsi vijana wanavyoweza kujiajiri kupitia fani ya sanaa.

Katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram, alikuwa na jumla ya wafuasi (followers) 457K na alikuwa ameweka jumla ya posti 39,583.

Uwezo wake wa kuchekesha, kuunganisha watu na kuacha tabasamu kwa maelfu ya watu katika sherehe mbalimbali, ulimfanya kuwa kielelezo cha vijana waliofanikiwa kujenga biashara imara kupitia talanta.

Msiba huu umegusa nyoyo za wadau wengi wa sanaa, ndugu, jamaa, na marafiki, ambao wanaendelea kutoa pole kwa familia ya marehemu Emmanuel Mathias.

Mungu ailaze roho ya Marehemu Emmanuel Mathias (MC Pilipili), MC wa Taifa, mahali pema peponi. Amina.

 

No comments