JKT Queens yapaa Misri kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika
JKT Queens imeondoka leo kwenda Misri kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya Wanawake inayotarajiwa kuanza kesho hadi Novemba 21.
Kikosi hicho kitaondoka na watu 43, wakiwemo wachezaji 23 na 20 ni benchi la ufundi na utawala.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Ofisa Habari wa JKT Queens, Masau Bwire alisema timu hiyo imekamilisha maandalizi yote na wachezaji wako tayari kiakili na kimwili kwa ajili ya michuano hiyo ya Afrika.
Alisema lengo la klabu ni kushindana kwa nguvu, kupata matokeo mazuri na kusonga mbele hadi fainali za mashindano hayo.
"Maandalizi yetu yamekamilika na wachezaji wamehamasika na wako tayari. Tunaomba kuungwa mkono na maombi ya Watanzania tunapoelekea Misri kutimiza malengo yetu," alisema.
JKT Queens wamepangwa Kundi B, ambapo watamenyana na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Aces Mimosas ya Ivory Coast na Gaborone United ya Botswana.
Wataanza dhidi ya Gaborone United, kabla ya kucheza na Aces Mimosas na watahitimisha mechi zao za hatua ya makundi kwa kumenyana na TP Mazembe.
Mabingwa hao wa Tanzania Bara wanataka kujionesha katika hatua ya bara na kuinua hadhi ya nchi katika soka la wanawake.

Post a Comment