Kikosi cha Gamondi hiki hapa, Kelvin aitwa
KAIMU Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi ameita wachezaji 23 kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) dhidi ya Kuwait utakaochezwa Novemba 14, Cairo nchini Misri.
Gamondi amemrejesha kundini mshambuliaji Kelvin John anayekipiga katika klabu ya Aalborg ya Denmark, huku akiwaacha washambuliaji wakongwe Mbwana Samatta anayechezea klabu ya Le Havre ya Ligi Kuu Ufaransa na Simon Msuva anayecheza Iraq.
Kikosi hicho kitaingia kambini Novemba 10, mwaka huu kujiandaa kwa mchezo huo ambao ndio kibarua cha kwanza cha Gamondi.
Gamondi ambaye pia ni Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Novemba 4, mwaka huu alitangazwa kukaimu nafasi iliyoachwa na Hemed Suleiman ‘Morocco’ aliyesitishiwa mkataba.
Raia huyo wa Argentina ataanza kuiongoza Taifa Stars katika mechi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Al Salam jijini Cairo nchini Misri, kuanzia saa 3:00 usiku.
Katika viwango vya FIFA, Tanzania inashika nafasi ya 107, wakati Kuwait inashika nafasi ya 135.
Wachezaji walioitwa ni makipa Yakoub Suleiman (Simba), Hussein Masalanga (Singida BS) na Zuberi Foba (Azam FC).
Mabeki ni Bakari Mwamnyeto (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Mohamed Hussein (Yanga), Alphonce Mabula (Shamakhi, Azerbaijan), Wilson Nangu (Simba), Pascal Msindo (Azam FC), Haji Mnoga (Salford City, Uingereza) na Dickson Job (Yanga).
Viungo ni Mudathir Yahya (Yanga), Novatus Dismas (Göztepe FC, Uturuki), Ibrahim Abdulla (Yanga), Habibu Idd (Singida BS), Tarryn Allarakhia (Rochdale AFC, Uingereza), Charles M'mombwa (Floriana FC, Malta), Feisal Salum (Azam FC).
Washambuliaji ni Suleiman Mwalimu (Simba), Morice Abraham (Simba), Abdul Suleiman (Azam FC), Paul Peter (JKT Tanzania) na Kelvin John (Aalborg BK, Denmark)

Post a Comment