Matokeo mabaya yamng'oa kocha Dimitar Pantev na wasaidizi wake Simba


Matokeo yasiyoridhisha na changamoto zilizojitokeza katika michezo ya hivi karibuni ndiyo sababu kuu iliyopelekea Uongozi wa Klabu ya Simba kufikia makubaliano ya pande mbili ya kusitisha mkataba na Meneja Mkuu, Dimitar Pantev, pamoja na wasaidizi wake wawili.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi imethibitisha kuwa mchakato wa kumtafuta kocha mwingine unaendelea, na kwa sasa, Kocha Seleman Matola atakuwa ndiye anayeongoza kikosi.

Katika kipindi hiki cha mpito, Matola ataiongoza Simba katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwamo dhidi ya Mbeya City, mchezo unaotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.

Pantev, raia wa Bulgaria mwenye umri wa miaka 49, aliwasili Simba akitokea Gaborone United ya Botswana, akirithi mikoba iliyoachwa wazi na Fadlu Davids aliyejiunga na Raja Casablanca ya Morocco. Kocha huyo anayemiliki leseni ya juu ya ukocha ya UEFA, alianza vizuri Ligi Kuu Tanzania Bara akiongoza Simba kushinda mechi zote.

 Rekodi ya Pantev Kimataifa

Changamoto kubwa kwa Pantev imekuwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Ameiongoza Simba katika michezo mitatu ya mashindano hayo:

Sare moja (0-0) dhidi ya Gaborone United kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kupoteza mechi mbili za hatua ya makundi ya Atlético Petróleos de Luanda (1-0) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na Stade Malien (2-1) ugenini.



No comments