Afrika yahitaji waandishi mahiri kukuza sayansi, teknolojia na ubunifu
Bara la Afrika lina uhitaji mkubwa wa waandishi wa habari waliobobea katika masuala ya sayansi. Uandishi mahiri ni nyenzo muhimu ya kufikisha ujumbe sahihi, huku ukisaidia kukuza maendeleo ya tafiti na uvumbuzi barani.
Kauli hiyo imetolewa na Profesa Blade Nzimande, Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Afrika Kusini, alipokuwa akifungua rasmi Mkutano wa 13 wa Waandishi wa Habari za Sayansi Duniani (WCSJ2025) jijini Pretoria. Mkutano huu, unaofanyika kuanzia Disemba 1-5, 2025, unalenga 'Uandishi wa sayansi, unaojenga uelewa na uthabiti wa sayansi na haki za kijamii'.
"Kazi yoyote ile tunayoifanya katika sayansi ina maana tu pale inapofahamika vizuri kwa watu na jamii nzima," alisema Prof. Nzimande. Alisisitiza kuwa waandishi wa habari ni daraja muhimu la kuielimisha jamii, si tu kutoa taarifa, bali pia kufanikisha Mkakati wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Afrika (STISA 2034) unaolenga kukuza utafiti na maendeleo barani.
Waziri huyo aliwahimiza waandishi wa habari kupambana na dhana potofu na ubaguzi, akisisitiza kuwa sayansi lazima iwe mradi unaoeleweka na watu wote, na si mradi wa tabaka la juu au la viongozi wachache. Alihimiza umuhimu wa kuhusisha makundi yaliyotengwa, ikiwemo wanawake, ili nao wawe sehemu ya mawasiliano ya kisayansi.
Changamoto nyingine kubwa inayowakabili waandishi wa habari za sayansi ni taarifa za uongo (fake news), hasa kupitia mitandao ya kijamii. Prof. Nzimande aliwakumbusha jinsi taarifa za uongo zilivyosambaa wakati wa COVID-19. "Mnapaswa kuwa jasiri na msiogope kuuliza maswali makubwa na muhimu," alisema, akisisitiza umuhimu wa kupambana na uzushi unaoweza kusababisha madhara makubwa.
Waziri huyo alieleza umuhimu wa kuingiza teknolojia mpya, kama Akili Bandia (AI), katika kazi za uandishi ili kuimarisha weledi. Pia, aliwataka waandishi kuchukua jukumu la kuhakikisha ubunifu, uvumbuzi, na miradi ya sayansi kutoka Afrika inatambulika ndani na nje ya bara, na hivyo kukuza diplomasia ya sayansi. "Bila ninyi, hatuwezi kuwafikia wale tunaopaswa kuwafikia," alihitimisha Prof. Nzimande.
Post a Comment