DK SAMIA AAGIZA MATOKEO YA HARAKA SIKU 100

 


Na MwandishiWetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka msisitizo mkubwa kwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wateule kuanza kazi kwa kasi na kuleta matokeo ya haraka kwa wananchi.

Aidha, kiongozi huyo wa nchi amewaagiza Mawaziri na Naibu Mawaziri hao kushirikiana na Makatibu Wakuu wa Wizara zao kuanza mara moja utekelezaji wa ahadi za siku 100 ili wananchi waanze kuona matokeo mazuri ndani ya muda huo mfupi.

Pia Rais Dkt. Samia amebainisha kuwa katika kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali itapunguza utegemezi kwenye mikopo na itaongeza nguvu katika kutumia rasilimali za ndani kutekeleza miradi yake. Lengo la hatua hii ni kuhakikisha kasi ya maendeleo haiathiriwi na mabadiliko ya upatikanaji wa fedha kutoka nje.

Sababu za kujikita ndani

Akizungumza baada ya kuwaapisha mawaziri 27 na Naibu mawaziri 29 katika Ikulu ya Chamwino, Rais Samia alisema changamoto iliyopo ni uchache wa rasilimali fedha za ndani na kuwataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele katika kutafuta fedha za ndani ili kutekeleza miradi hiyo.

“Changamoto inayotukabili ni rasilimali, rasilimali zetu ni chache, kama mnavyojua mara nyingi tunategemea kupata kutoka nje, mikopo kutoka kwa taasisi mbalimbali za kimatifa na benki za kimataifa,” alisema.

Aliongeza: “Lakini yaliyotokea (vurugu wakati wa uchaguzi) nchini kwetu yametutia doa kidogo na huenda yakatupunguzia sifa ya kupata hiyo mikopo kwa urahisi kama tulivyopata muhula wa kwanza wa awamu ya sita, muhula wa kwanza tulikuwa tunapata sana, kwa sifa zetu, kwa msimamo wetu na kwa kazi tunazofanya, lakini doa tulilojitia linaweza likaturudisha nyuma.”

“Kwa maana hiyo tuna kazi ya kutafuta fedha humu ndani, kutumia rasilimali zetu alizotupa Mungu, tutaangalia njia gani tutazitumia tupate fedha ili tutekeleze miradi ambayo tunakwenda kuitekeleza,” alieleza.

Rais Samia alisisitiza kuwa muhula wa pili wa uongozi wake, serikali imejipanga kuanza kutekeleza miradi kwa fedha za ndani bila kusubiri za wahisani.

“Kubwa zaidi muhula wa pili wa awamu ya sita tutaanza kufanya miradi wenyewe halafu mashirika yatatukuta njiani, hatutakaa tusubiri, tunauza mradi na kwenda kubembeleza kukiwa na masharti mengi, badala ya kupata mkopo kwa miezi mitatu au minne unachukua mwaka mzima tunabembeleza mradi mmoja mpaka kibali kinatoka tuna miaka miwili tumemaliza. Hatutasubiri hayo, tutaanza kwa fedha ya ndani halafu… watatukuta katikati, huo ndio mwelekeo,” alisema.

Rais Samia alisisitiza kuwa miaka mitano si midogo lakini si mingi sana, na hataona shida kubadilisha ..." Na mnanijua…nitabadilisha mpaka nimpate yule aliye tayari kufanya kazi na mimi kwa moyo mkuu na kwa moyo mmoja.”

Katika hotuba yake, Rais Samia aliwashukuru waliokuwa mawaziri katika muhula wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanya kazi zilizoleta maendeleo.

"Lakini kazi ni kupishana, tuna timu mpya kongwe wamechanganyika tukaendeleze mapambano ya kuwaletea maendeleo wananchi,” alisema.

Rais Samia alisema leo kutakuwa na kikao kazi cha viongozi hao ambapo masuala mbalimbali wataelezwa kuhusu hali ya uchumi, rasilimali na mikakati ya kitaifa.

Maoni ya mawaziri


Baadhi ya Mawaziri walioapishwa walitoa maoni yao kuhusu maagizo hayo.

Judith Kapinga (Waziri wa Viwanda): Alisema agizo la kutumia fedha za ndani limewapa angalizo na kuwatoa hofu Watanzania, akisisitiza kuwa, "Wizara ya Viwanda ni injini ya uchumi... ni lazima tuendelee kukimbia kwa kutumia akili na maarifa yetu."

Regina Ndege (Naibu Waziri, Utumishi na Utawala Bora): Alisema tafsiri ya Kazi na Utu ndiyo kipimo kikubwa cha utumishi, akitaka viongozi kufanya kazi kwa ushirikiano na kutotanguliza maslahi binafsi.

Jumaa Aweso (Waziri wa Maji): Alisema agizo la Rais la kutaka mawaziri wakimbie linamlazimu kutimiza yaliyoagizwa kwa nguvu na maarifa zaidi, akiamini milango ya utekelezaji wa miradi itafunguka.

No comments