DK NCHIMBI: TANZANIA NI SALAMA NA TULIVU TUPO TAYARI KUENDELEA KUPOKEA WAGENI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan imechukua hatua za kurejesha utengamano katika nchi na
kuhakikisha wananchi wanaishi katika utawala wa sheria.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akimwakilisha Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano
wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC), uliyofanyika kwa njia ya mtandao, akiwa
mkoani Dodoma.
Amesema dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni
kuhakikisha mchakato wa mazungumzo ya maridhiano unafanikiwa ili kuwa na Taifa
lenye amani na umoja na kuendelea kuwa mfano wa utulivu katika Afrika na Dunia
kwa ujumla.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema Tanzania ni
salama na tulivu na ipo tayari kuendelea kupokea wageni kutoka duniani kote kwa
manufaa ya nchi zote.
Aidha, Makamu wa Rais, amewashukuru viongozi wa SADC
walioshiriki uapisho wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wote waliotoa
pongezi za dhati. Amesema jitihada zote zitatumika kuhakikisha Tanzania inapata
maendeleo na amani kuendelezwa.
Mkutano huo umempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushindi aliyoupata na uchaguzi wenye
mafanikio.
Mkutano huo ulilenga kujadili kujiondoa kwa nchi ya
Madagascar kama nchi Mwenyekiti wa SADC, ambapo nchi ya Afrika Kusini
imependekezwa kuwa Mwenyekiti kwa kipindi cha mpito mpaka kufikia mwezi Agosti
2026.
Mkutano huo umekubaliana kuendelea kutumia kauli mbiu
ya Mkutano wa 45 wa SADC uliyofanyika nchini Madagascar ambayo ni “Kuimarisha
Viwanda, Mapinduzi ya Kilimo, Mabadiliko ya Nishati kwa SADC yenye Uhimilivu”





Post a Comment