WAKATI Simba
ikitua Mtwara kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu, Tanzania Bara unaotarajiwa
kuchezwa kesho, kocha wa Ndanda FC, Malale Hamsini amesema hana hofu na wachezaji
wa kigeni wa Simba.
Akizungumza Malale alisema anatambua mchezo ni dakika 90 japo mchezo ni mgumu kwa
kila upande lakini wamejipanga kwa ajili ya ushindi.
“Sina hofu na wachezaji wa kigeni wa Simba
ninachotambua mchezo wa soka ni dakika 90, hii mechi ni ngumu kila upande kwetu
na kwao pia. Tumejipanga kwa ajili ya ushindi na hii sio kwa Simba pekee bali
mechi yoyote iliyopo mbele yetu ni kama fainali,” alisema Malale.
Pia Malale aliwataka mashabiki na wanachama wa Ndanda
kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao katika mechi hiyo kwani itasaidia
kuwapa morali wachezaji kupata ushindi.
Simba iliwasili Mtwara juzi huku Kocha Msaidizi Djuma
Masoud akisema ushindi ni muhimu ili kuwapa mashabiki zawadi ya mwaka mpya
baada ya kuondolewa kwenye kombe la FA na Green Warriors.
Ndanda haina nyota wa kigeni tofauti na Simba ambao
wamesajili nyota wa kigeni akiwemo James Kotei, Laudit Mavugo, Juuko Murshid,
Haruna Niyonzama lakini Malale ameonyesha ‘kiburi’ kuwa nyota hao ni wa kawaida
kwake.
Katika
mchezo huo Simba itawakosa wachezaji Kipa Said Mohamed ‘Nduda’ na Salim Mbonde na Shomari Kapombe ambao ni
majeruhi huku beki mpya Asante Kwasi akiachwa Dar es Salaam aendelee kujifua
kwa ajili ya mashindano ya Mapinduzi
Kwasi atajiunga na timu itaporejea kutoka Mtwara kwa safari ya Zanzibar
kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ambapo Simba imepangwa Kundi A kwenye
Kombe la Mapinduzi pamoja na Azam FC, URA ya Uganda, Jamhuri na Mwenge ambao
watafungua nao pazia
Kwa sasa Simba inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 23 baada ya
kushuka dimbani mara 11 lakini Azam FC inaweza ikawa kileleni endapo itashinda
mchezo wake dhidi ya Stand United.
No comments:
Post a Comment