KATIBU MKUU UN TOURISM AIMWAGIA SIFA TANZANIA



Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UN Tourism), Bi. Shaikha Al Nuwais, ameipongeza Tanzania kama mmoja wa vinara wa utalii duniani huku akimuelezea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kama chapa imara ya kimataifa ya nchi yake. 

Akizungumza katika mkutano wa pande mbili uliofanyika jijini Dubai, Bi. Shaikha amebainisha kuwa filamu ya 'Tanzania: The Royal Tour' imekuwa na athari chanya sana katika kuvutia watalii na amethibitisha utayari wa shirika lake kuunga mkono azma ya Tanzania ya kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni nane. 

Aidha, Katibu Mkuu huyo ameeleza kuwa UN Tourism ipo tayari kuisaidia Tanzania kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika Pato la Taifa kutoka asilimia 17 hadi asilimia 24, kutoa msaada wa kitaalamu, pamoja na kuunga mkono utayari wa Tanzania kuwa mwenyeji wa Ofisi ya Kanda ya shirika hilo.

Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amempongeza Bi. Shaikha Al Nuwais kwa kuchaguliwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo ya juu na kuthibitisha dhamira ya Tanzania ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na shirika hilo. 

Rais Samia amebainisha kuwa Tanzania inalenga kuibadilisha sekta ya utalii kupitia uendelevu, ubunifu, na teknolojia ya kidijitali, ikiwemo kuimarisha mifumo ya utalii unaotegemea jamii katika maeneo ya Zanzibar na Kisiwa cha Mafia. Mazungumzo hayo yamejikita pia katika utofauti wa bidhaa za utalii kama utalii wa michezo kwa kuzingatia michuano ya AFCON 2027, utalii wa utamaduni, na utalii wa vyakula, yote yakilenga kutengeneza ajira hususan kwa vijana na wanawake.



Katika mkutano mwingine wa ngazi ya juu, Rais Samia amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Antigua na Barbuda, Mheshimiwa Gaston Browne, ambapo wamejadili kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na Karibiani kupitia mfumo wa Jumuiya ya Madola. Rais Samia amemuelezea Waziri Mkuu Browne hatua ambazo serikali yake inachukua kuimarisha utawala nchini, zikiwemo kuanzishwa kwa Tume ya Uchunguzi, mipango ya kuunda Tume ya Maridhiano ya Kitaifa, na maandalizi ya marekebisho ya Katiba. Viongozi hao wamekubaliana kuendeleza ushirikiano katika maeneo ya biashara, uwekezaji, utalii, usalama, na muunganisho wa usafiri wa anga kati ya mabara hayo mawili.

Waziri Mkuu Gaston Browne amempongeza Rais Samia kwa uongozi wake na uwazi katika kushughulikia masuala ya kiusalama na utawala wa kikatiba nchini Tanzania. Browne amemwalika rasmi Rais Samia kushiriki Mkutano ujao wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) na kutangaza nia yake ya kuitembelea Tanzania mwezi Juni au Julai, 2026. Rais Samia amethibitisha utayari wa Tanzania kuunga mkono Uenyekiti wa Jumuiya ya Madola wa Antigua na Barbuda, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi inayotekeleza makubaliano kwa vitendo.

Mazungumzo haya ya pande mbili yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Serikali (WGS 2026) yanaakisi mkakati mpana wa Tanzania wa diplomasia ya kiuchumi inayolenga matokeo halisi. Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushikamana na misingi ya amani, uwazi, na ushirikiano wa kimataifa ili kuvutia uwekezaji wenye tija na kuliweka taifa katika taswira ya mshirika wa kuaminika kulingana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

No comments