KAMATI ya Bodi ya Ligi Kuu ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi
imemfungia kocha wa Azam FC, Aristica Cioaba kwa mechi tatu na faini ya sh.
500,000 kwa kosa la kuwabughudhi waamuzi katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting
iliochezwa Novemba 4, 2017 katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam
Akizungumza leo Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura alisema
Cioaba aliwafuata waamuzi na kuwalalamikia kwa kurusha mikono
akionyesha kutoridhika na maamuzi yao.
“Adhabu ya Cioaba imezingatia Kanuni ya 40(1) ya Ligi
Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha na Tanzania Prisons
imepewa onyo kali kwa kuwakilishwa kwenye benchi na ofisa tofauti na yule
aliyeudhuria kikao cha maandalizi,” alisema Wambura.
Wambura alisema Tanzania Prisons iliwakilishwa na Meneja
wake Erasto Ntabah lakini kwenye benchi alikaa Hassan Mtege katika mchezo dhidi
ya Kagera Sugar uliochezwa Novemba 4 kwenye Uwanja wa Kaitaba Kagera
“Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya
Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo na Ntabah amesimamishwa hadi suala lake la
kutoka jukwaani na kwenda kumfokea mwamuzi wa akiba litakaposikilizwa na Kamati
ya Nidhamu ya TFF,” alisema Wambura
Pia Wambura alisema mchezaji wa Tanzania Prisons Benjamin
Asukile amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kutolewa
nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kiwiko kwenye paji la uso mchezaji wa
Kagera Sugar.
Hata hivyo uongozi wa Azam FC umesema unasikitishwa na
kitendo cha Kamati hiyo kumfungia kocha Cioaba bila kuwapa taarifa.
“Tunasikitika kusikia habari za kufungiwa kocha kupitia
vyombo vya habari, tulipaswa kutaarifiwa kiofisi kabla ya kutangazwa kwenye
vyombo vya habari,” alisema Msemaji wa Azam FC, Jaffa Idd.
No comments:
Post a Comment