SIMBA, Yanga
na Azam FC kesho zitashuka dimbani kwenye viwanja tofauti kusaka pointi tatu
ambazo zitaendelea kuwapa nafasi ya kuendelea kuingia katika vita ya ubingwa,
kila mmoja akionyesha shauku na umuhimu wa kushinda ugenini.
Wekundu hao
watakuwa kwenye uwanja wa Uhuru dhidi ya African Lyon, ikijivunia kushika
usukani wa ligi kwa pointi 35 na kuziacha Yanga na Azam kwa tofauti ya pointi
nane hadi 13.
Simba
haijapoteza mchezo hata mmoja katika 13 iliyocheza, ikishinda 11 na kupata sare
mbili. Mbali na rekodi hiyo bora, pia, ndio timu yenye mchezaji anaongoza kwa
ufungaji Shiza Kichuya akiwa na magoli tisa.
Timu hiyo
ina nafasi kubwa ya kushinda mchezo wa leo baada ya kutoka kushinda dhidi ya
Stand United bao 1-0, uliochezwa Shinyanga hivi karibuni.
Inacheza na African Lyon ambayo licha ya
kutokuwa katika nafasi nzuri bado haipaswi kudharauliwa kwa kuwa
haitabiriki. Timu hiyo ina pointi 14
katika michezo 14 iliyocheza ikishika nafasi ya 11.
Yanga
itakuwa kwenye uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya. Ni timu inayoshika nafasi ya
pili ikiwa na pointi 27 katika michezo 13 iliyocheza. Mchezo wa leo una umuhimu
mkubwa kwao kushinda kama inataka kukimbizana na Simba katika mbio za ubingwa.
Mchezo huo
hautakuwa rahisi kwa kila timu, kwani zote zimetoka kupoteza michezo yao, Yanga
ikitoka kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons ikifungwa na
Ndanda FC bao 1-0.
Kuanzia
msimu wa 2013 hadi sasa, Yanga imekuwa na rekodi nzuri ya kufunga au kutoka
sare dhidi ya Prisons, lakini Februari mwaka huu kwenye uwanja wa Sokoine, timu
hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.
Aidha, Azam
FC itakuwa kwenye uwanja wa CCM, Kirumba Mwanza ikichuana na Mbao FC. Timu hii
imeanza kurudi taratibu baada ya kushinda michezo miwili iliyopita ya ugenini.
Iliifunga 1-0 Toto Africans na 3-2 Kagera Sugar.
Katika
michezo 13 iliyocheza imeshinda sita, sare nne na kufungwa mitatu ikishika
nafasi ya 13 kwa pointi 22. Inakutana na Mbao FC ambayo imekuwa ikizikazia timu
kubwa licha ya kufungwa.
Mbao licha
ya kutokuwa na uzoefu wa kutosha wa ligi, inapokutana na timu kubwa hucheza
mchezo mzuri wa kujihami na kushambulia mara chache na mara unapoidharau ni
rahisi kuabisha kwani ina wachezaji wanaojituma.
Timu hii
bado haiko katika nafasi nzuri baada ya kupoteza michezo kadhaa iliyopita ikiwa
ugenini. Inashika nafasi ya tatu kutoka mwisho, ikiwa na pointi 12 katika
michezo 14.
Ndanda FC
inayoshika nafasi ya 10 kwa pointi 16
itaikaribisha Stand United. Huu utakuwa mchezo mgumu kwa kila timu kwani
timu hiyo ya Mtwara ni mara chache imefungwa kwenye uwanja wake msimu huu.
Pia, Stand ni timu ambayo imekuja kivingine, iko
vizuri na kwa sasa inashika nafasi ya nne, ikiwa na pointi 22 katika michezo 14
iliyocheza. Ni mchezo ambao iwapo Stand itakubali kichapo itashuka na zile
zilizoko chini yake kama zikishinda zina uwezekano wa kupanda, hivyo utakuwa
mgumu.
Kagera Sugar
itakutana na Ruvu Shooting huko Kaitaba. Kagera inashika nafasi ya tano ikiwa
na pointi 21 na Ruvu nafasi ya saba kwa pointi 19. Kila mmoja anahitaji ushindi
kujisogeza kutoka safasi moja hadi nyingine.
JKT Ruvu
itaikaribisha Toto Africans. Timu zote mbili zinafuatana kwa kushika mkia
wakitofautiana kwa pointi moja. JKT ina pointi 12 na Toto 11 wote wakiwa
wameshacheza michezo 14. Hii ni mechi inayohitaji ushindi kwa kila mmoja
kujiondoa katika nafasi walizopo.
No comments:
Post a Comment