Kikao cha
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kilichoketi jumanne ya tarehe 24, Machi 2015
jijini Dar es salaam, kimepitia taarifa mbalimbali za michezo iliyochezwa na
kutoa adhabu kwa wachezaji na vilabu vya Ligi Kuu ya Vodacom.
Katika mechi
namba 107 iliyowakutanisha wenyeji Ndanda FC dhidi ya Coastal Unioni, klabu ya Ndanda
imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi
Kuu ya Vodacom kutokana na washabiki
wake kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi Anold Bugado.
Mechi namba
108 iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, (Stand United dhidi Simba
SC), wenyeji timu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa
mujibu wa Kanuni ya 14(8) kutokana na timu yake kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika
ishirini.
Mchezo namba
117 uliozikutanisha Simba SC dhidi ya Yanga SC kwenye Uwanja wa Taifa jijini
Dar es salaam, timu ya Simba imepigwa faini
ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(9) kwa kukataa kuingia kwenye
vyumba vya kubadilishia nguo.
Nayo klabu ya Yanga
imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(11) baada ya
timu yake kuonyeshwa kadi zaidi ya tano kwenye mchezo dhidi ya Simba SC, huku
mshambualiji wake Dany Mrwanda akipigwa
faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(12) kwa kutopeana mikono
na wachezaji wa timu hiyo.
Mchezaji Haruna
Niyonzima wa Yanga amepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni
ya 37(f) kwa kupiga teke meza ya
mwamuzi wa akiba baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Suala la
mshambuliaji wa Yanga Amissi Tambwe kumshika korodani beki wa Simba SC Murshid Juuko
limepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu.
Kipa wa timu
ya Simba SC, Ivo Mapunda amepewa onyo kwa kufunika tangazo la mdhamini wa Ligi
Kuu (Vodacom) kwa kutumia taulo lake wakati
wa mechi dhidi ya Yanga, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake iwapo
atarudia kufanya tukio la aina hiyo.
Nao wachezaji Salum
Abubakar wa Azam FC na Richard Maranya wa JKT Ruvu wamepigwa faini ya sh.
500,000 (laki tano) kila mmoja na kusimamishwa mechi tatu kwa mujibu wa Kanuni ya
37(3) kwa kupigana uwanjani kwenye mechi namba 123 ambapo walitolewa nje kwa kadi
nyekundu.
Klabu ya Kagera
Sugar imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(9)
baada ya timu yake kugoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwenye
mchezo namba 130 dhidi ya Young Africans uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.
Mechi namba
132 iliyozikutanisha Azam na Ndanda SC kwenye uwanja wa Chamazi, klabu ya Ndanda
imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) baada ya
washabiki wake kuwamwagia maji na kuwarushia chupa za maji washabiki wa Azam.
Aidha klabu ya
Stand United imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa mujibu wa Kanuni ya
14(8) kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi namba 134 dhidi ya timu ya
Mbeya City, pia imepigwa faini ya sh.
500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(9) kwa kutoingia kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo kwenye mchezo huo.
Kiongozi wa
Stand United, Muhibu Kanu amepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu baada ya kuondolewa
kwenye benchi na mwamuzi wa mchezo dhidi ya Mbeya City kutokana na kutumia lugha
ya kuhamasisha vurugu kwa timu yake na kupinga uamuzi wa refarii.
Katika mchezo
namba 135 uliochezwa jijini Tanga na kuwakutanisha wenyeji Mgambo Shooting
dhidi ya Yanga SC, Yanga SC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu
wa Kanuni ya 42(1) kutokana na washabiki wake kuvamia uwanja baada ya mechi namba
135 dhidi ya Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
No comments:
Post a Comment