FURSA KWA WABUNIFU: JIOPAKI YA NGORONGORO NI MGODI WA MAUDHUI
Wakati ulimwengu wa kidijitali ukizidi kutawaliwa na maudhui ya kigeni, vijana wabunifu nchini Tanzania wameaswa kugeukia urithi wa asili kama chanzo cha malighafi ya hadithi, filamu za katuni (animations), na michezo ya video.
Makumbusho ya Jiopaki ya Ngorongoro-Lengai yaliyopo Karatu, mkoani Arusha, yamebainika kuwa si kituo cha kitalii tu, bali ni 'migodi' ya maarifa inayoweza kuwapa wabunifu wetu maudhui ya kipekee yatakayoweza kushindana katika soko la kimataifa.
Kwa watengeneza maudhui ya kidijitali na waandaaji wa filamu za katuni, Jiopaki hii inatoa taswira ya kipekee ya jinsi dunia ilivyokuwa maelfu ya miaka iliyopita. Badala ya kuiga hadithi za mazimwi au mashujaa wa mataifa ya mbali, wabunifu wanaweza kutumia teknolojia ya sauti za wanyama na simulizi za kijiolojia zilizopo hapo kutengeneza hadithi zenye asili ya Kitanzania. Taswira ya milima iliyozaliwa na volkano na chimbuko la binadamu ni misingi tosha ya kuandaa maandiko ya filamu (scripts) yanayohusu maisha ya kale, uvumbuzi, na mabadiliko ya mazingira.
Upekee wa Jiopaki ya Ngorongoro-Lengai unatoa fursa kwa waandishi wa hadithi fupi na vitabu vya watoto kuchota hekima za kale na kuzichanganya na sayansi ya kisasa. Kwa kutembelea eneo hili, mbunifu anaweza kuelewa kwa kina jinsi asili yetu ilivyojengwa, jambo litakalosaidia kutengeneza maudhui yenye uhalisia (authenticity). Hili ni soko ambalo bado halijaguswa kikamilifu nchini, ambapo watoto wetu wanaweza kuanza kuona katuni zinazozungumzia maajabu ya Olduvai Gorge au milima ya volkano ya kaskazini mwa Tanzania.
Aidha, gharama nafuu zilizowekwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)—ambapo kijana analipa Sh 5,900 pekee—ni mwaliko rasmi kwa wabunifu wenye mitaji midogo kufanya tafiti (research) za kutosha. Mbunifu anayefika hapa haji kama mtalii wa kawaida, bali anakuja kama mtafiti anayetafuta "dhahabu ya maudhui" itakayomfanya atoke kimaisha. Teknolojia ya kisasa iliyopo makumbusho hayo tayari imeweka msingi wa jinsi sayansi na sanaa zinavyoweza kuungana kuvutia hadhira.
Wito unatolewa kwa vyama vya wabunifu, waongozaji wa filamu, na wasanii wa michoro ya kompyuta (graphic designers) kuandaa ziara za mafunzo katika kituo hiki cha kipekee.
Takwimu zilizotolewa na Ofisa Uhifadhi Mkuu na Msimamizi wa Makumbusho hayo kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Dkt. Agness Gidna, zinaonesha kuwa Watanzania ndio wateja wakuu wa kivutio hicho kwa sasa. Katika mwezi Novemba pekee, kati ya watu 575 waliotembelea, Watanzania walikuwa 568, huku mwezi Januari mwaka huu idadi ikiwa ni Watanzania 451 kati ya wageni 463. Mwitikio huu unatajwa kama ushindi kwa utalii wa ndani, ukidhihirisha kuwa wananchi wameanza kuthamini na kuwekeza katika kujifunza tunu za nchi yao.
Makundi yanayoongoza kwa kutembelea makumbusho hayo ni pamoja na wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, vyuo, pamoja na makundi ya kijamii kama SACCOS na jamii za kikabila zinazoishi mbali na asili yao. Kivutio kikubwa kwa wageni hao kimekuwa ni matumizi ya teknolojia ya kisasa ya sauti za wanyama, uwezo wa kuendesha baiskeli ndani ya makumbusho, na ukumbi wa utamaduni unaotoa taswira pana ya maisha ya kale. Kwa wanafunzi, eneo hilo limekuwa darasa muhimu la kisayansi linaloezea jinsi volkano ilivyounda mabonde na milima ya Ngorongoro, pamoja na historia ya chimbuko la binadamu.
Kwa kufanya hivyo, Tanzania haitakuwa tu taifa linalotumiwa maudhui kutoka nje, bali itakuwa kitovu cha hadithi za asili zinazotumia teknolojia ya kisasa kuelezea maajabu ya Jiopaki ya pili kwa ukubwa Afrika. Ni wakati wa vijana wetu kuacha 'kufikiria nje ya boksi' na badala yake kuanza 'kujenga boksi lao' kutokana na urithi wa Ngorongoro-Lengai.

Post a Comment