WACOMORO ni wateja wazuri kwa Yanga
na hawana ujanja wa kufurukuta kwa namna yoyote mbele ya timu hiyo ya Dar es Salaam.
Hivyo ndivyo unavyoweza kuzungumzia
matokeo ya mchezo wa kwanza hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya
Yanga na Komorozine ya Comoro uliofanyika leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 7-0.
Yanga iliyoenda mapumziko ikiwa
mbele kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mrisho Ngassa dakika ya 13 na Nadir Haroub
dakika ya 20 ilitawala sehemu kubwa ya mchezo huo, huku wapinzani wao
wakionekana wachovu.
Ngassa alifunga bao hilo kwa kichwa
akiunganisha krosi ya Mbuyu Twite, huku bao la Haroub pia likifungwa kwa kichwa
kutokana na krosi ya David Luhende.
Kipindi hicho cha kwanza Yanga
walifika mara kadhaa langoni kwa Komorozine, lakini Hamisi Kiiza, Ngassa, Simon
Msuva na Haruna Niyonzima walishindwa kutumia vyema nafasi walizozipata, huku
Wacomoro wenyewe wakishindwa kufanya mashambulizi ya hatari.
Yanga walibadilika kipindi cha pili
na kufanya mashambulizi yalizaa mabao ya haraka haraka yaliyofungwa na Didier
Kavumbagu dakika ya 57 kabla ya Hamisi Kiiza kufunga la nne dakika ya 59.
Ngassa alifunga mabao mawili ya
haraka haraka dakika za 64 na 68 hivyo kupiga hat-trick jana, wakati bao la
saba lilifungwa na Kavumbagu dakika ya 80.
Wacomoro hawakufanya mashambulizi ya
nguvu, hivyo kumfanya kipa Juma Kaseja wa Yanga kutokuwa na kazi kubwa.
Matokeo ya mchezo huo yamedhihirisha
ubabe wa Yanga kwa timu za Comoro, ambayo haina historia nzuri katika soka
kimataifa.
Komorozine inakuwa timu ya tatu
kukutana na Yanga kwenye michuano ya Afrika baada ya AJSM na Etoile d'Or
Mirontsy.
Januari 27, mwaka 2007 katika Ligi
ya Mabingwa Afrika, raundi ya awali Yanga iliifunga AJSM mabao 5-1 Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam na moja kwa moja kufuzu Raundi ya Kwanza, kwa sababu
hakukuwa na mchezo wa marudiano kwa kuwa Comoro hawakuwa na Uwanja wenye
kukidhi sifa za michuano ya Afrika.
Mwaka 2009, Yanga iliitoa timu
nyingine ya Comoro, Etoile de Mironsty kwa jumla ya mabao 14-1, ikianza kushinda
8-1 Januari 31 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kushinda 6-0
ugenini, wakati huo ikiwa chini ya kocha Mserbia, Dusan Kondic.
Hata hivyo mbio za Yanga ziliisha baada
ya kutolewa na mabingwa wa kihistoria Afrika, Al Ahly ya Misri kwa jumla ya
mabao 4-0, ikianza kufungwa 3-0 Machi 15 mjini Cairo na baadaye 1-0 wiki mbili baadaye Dar es
Salaam.
Kutokana na matokeo hao Yanga sasa
wanahitaji ushindi wowote, sare ama wasifungwe zaidi ya mabao 7-0 ili waingie
raundi inayofuata, ambapo watacheza na Ahly , ambao ndio mabingwa watetezi wa
Afrika.
Yanga: Juma Kaseja, Mbuyu
Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kevin Yondan/Rajab Zahir, Frank Domayo,
Simon Msuva/Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Hamisi Kiiza, Mrisho Ngassa na
David Luhende/Didier Kavumbangu.
Komorozine; Attoumani Farid, Ali Mohamed Mouhousoune,
Nizar Amir, Abdou Moussoidi Kou, Ahamadi Houmadi Ali, Moidjie Ali, Mourthadhoi
Fayssol, Attoumane Omar, Mohamed Erfeda/Imroina Ismael dk30, Mouyade Almansour
Nafouondi na Ahmed Waladi Mouhamdi/Ghaidane Mahmoud dk80.
No comments:
Post a Comment