Wapotoshaji mtandaoni hawana chao Mazungumzo ya Rais Samia na TEC ni Dhihirisho la Utamaduni wa Ushirikiano



Utamaduni wa Serikali kushirikiana na taasisi za dini nchini Tanzania si jambo jipya wala la kushangaza, bali ni msingi thabiti uliowekwa tangu enzi za Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Taasisi za dini zimekuwa washirika wakubwa wa maendeleo katika sekta muhimu kama vile afya, elimu, na huduma za jamii.

Mazungumzo yaliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Maaskofu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) yanaendeleza utamaduni huu adhimu wa kitaifa wa kushauriana, kusikilizana, na kuweka maslahi ya Taifa mbele.

Ni upofu wa kifikra kwa baadhi ya wachochezi kudai au kubeza kuwa mazungumzo haya ni ishara kwamba serikali "imebanwa na haifurukuti." Huu ni mtazamo finyu unaotokana na hamu ya kupotosha umma kwa malengo binafsi ya kisiasa. 

Katika utawala bora unaojali ustawi wa wananchi, serikali sikivu haitawali kwa ubabe au kujitenga na wadau wake muhimu, bali hutambua kuwa ujenzi wa taifa unahitaji nguvu za pamoja.

Kukutana kwa Rais Samia na viongozi wa dini kunadhihirisha serikali madhubuti, yenye hekima, inayothamini mchango wa taasisi za kidini katika kulea jamii yenye maadili mema, uwajibikaji, na mshikamano. Hii si alama ya udhaifu, bali ni uthibitisho wa utawala unaothamini maridhiano na ustawi wa jumla wa wananchi wake.

Mazungumzo haya yanajenga daraja imara la mawasiliano kati ya Serikali na jamii pana. Kwa kuwa taasisi za dini zina ukaribu mkubwa na wananchi na zinagusa maisha yao ya kila siku, ushauri na mitazamo yao inatoa picha halisi ya changamoto na matarajio ya wananchi. 

Dhamira ya Rais Samia ya kuendelea kushirikisha makundi mbalimbali inadhihirisha wazi kuwa Serikali haiwezi kujenga taifa peke yake, bali inahitaji mawazo, uzoefu, na ushiriki wa wadau wote ili kulinda amani na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo endelevu.

No comments