Serikali Yakamata Dhahabu ya Shilingi Bilioni 1.2 Iliyokuwa Ikitoroshwa



Wizara ya Madini imefanikiwa kukamata gramu 4,402.20 za dhahabu zenye thamani ya Shilingi 1,238,458,594.42 iliyokuwa inatoroshwa kwa njia za panya.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Madini Antony mavunde amesema mafanikio ya ukamataji huo umetokana na kuimarishwa kwa mfumo wa udhibiti kupitia Kikosi Kazi maalum kilichoundwa kwa kushirikiana na vyombo vya dola ili kudhibiti utoroshaji wa mali za Taifa.

Aidha, amebainisha kuwa dhahabu hiyo haikupitia katika mfumo rasmi wa kibiashara, hali inayotishia kuikosesha Serikali mapato yanayotakiwa kuelekezwa kwenye uboreshaji wa huduma za jamii.

Dhahabu hiyo imetaifishwa rasmi na kuhifadhiwa Benki Kuu ya Tanzania.

Waziri huyo ametoa  maelekezo kwa Kikosi Kazi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kufanya uchunguzi wa kina ili kumbaini mtuhumiwa alikotoka na alikokuwa anapeleka shehena hiyo, lengo likiwa ni kung’oa kabisa mzizi na kuvunja mtandao wa utoroshaji wa madini nchini.

Pamoja na hatua hizo, ameagiza kuwa iwapo mtuhumiwa aliyekamatwa alikuwa na leseni halali ya biashara, kibali hicho kifutwe mara moja na jina lake liwekwe kwenye orodha maalum ya wahalifu ili asiruhusiwe tena kujihusisha na shughuli za madini nchini.


No comments