Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Tuesday, August 20, 2013

KIPENGA CHA LIGI KUU BARA KIMEPULIZWA, NANI KUVUNA NINI MSIMU WA 2013/14

MCHEZO wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam FC iliyochezwa wikendi iliyopita Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa Yanga kupata ushindi wa bao 1-0, ilikuwa ishara ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara kuanza. DIMBA linatathmini timu zote 14 shiriki na nini kinachoweza kutokea mwishoni mwa msimu.

* Ashanti United
Msimu uliopita: Vinara Kundi B
Kocha: Mbaraka Mbaruka
Si wageni kwenye ligi ila wamerudi tena ambapo mara ya mwisho kushiriki Ligi Kuu Bara ilikuwa msimu 2007/08. Ashanti United inaongeza idadi ya timu za Dar es Salaam na ni mojawapo ya timu yenye mashabiki wengi. Uongozi wa Ashanti United umejitahidi kuwa makini kwenye usajili lakini kinachosubiriwa ni namna gani watakavyokabiliana na wapinzani wao.
MATARAJIO: Hawatataka kurudia makosa yaliyosababisha kushushwa daraja na dalili zinaonyesha watamaliza kwenye nafasi 10 za juu.

* Azam FC
Msimu uliopita: Nafasi ya pili
Kocha: Stewart Hall
Kinywani mwa wadau wa soka, Azam FC ni mfano mzuri wa namna gani klabu za soka zinapaswa kuendeshwa. Azam FC waliweka kambi nchini Afrika Kusini kujiandaa na msimu mpya ambapo walicheza na klabu kubwa huko wakishinda moja na kufungwa tatu. Kupoteza mchezo wa Ngao ya Jamii si kupoteza imani kwa timu hii kuelekea msimu mpya. Kocha Hall hajafanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha kwanza na amepandisha baadhi ya wachezaji waliokuwa kwenye kikosi cha vijana. Labda huu unaweza ukawa msimu wa mshambuliaji Gaudence Mwaikimba kurudisha makali yake. Hata hivyo, safu ya ushambuliaji inahitajika kuwa makini huku viungo wakicheza mpira wa kasi badala ya kuremba.
MATARAJIO: Kuna kila dalili huu unaweza ukawa msimu wa Azam FC kutwaa ubingwa baada ya misimu miwili mfululizo kumaliza nafasi ya pili.

* Coastal Union
Msimu uliopita: Nafasi ya sita
Kocha: Hemedi Moroko
Miongoni mwa timu ambazo zimetumia fedha nyingi kufanya usajili ni Coastal Union ambayo imejichimbia Tanga. Imewaongeza kundini kiungo Haruna Moshi ‘Boban’, beki Juma Nyosso, winga Uhuru Selemani, washambuliaji Mkenya Crispini Odula na Mganda Yayo Lutimba. Coastal Union imekuwa ikipata sapoti kubwa kutoka kwa wenyeji wa mkoa wa Tanga ambao hujitokeza kwa wingi kujaza Uwanja wa Mkwakani hivyo basi Moroko hatataka kuwaangusha kwa kuhakikisha ‘hatoki mtu’ Tanga.
MATARAJIO: Kama usajili ni kigezo cha timu kufanya vizuri, hamna shaka Coastal Union itamaliza kwenye nafasi nne za juu. 

* JKT Oljoro
Msimu uliopita: Nafasi ya nane
Kocha: Alex Mwangeja
Huu utakuwa ni msimu wa tatu tangu JKT Oljoro ipande daraja ambapo imekuwa ikiwakilisha vyema mkoa wa Arusha baada ya kushuka kwa timu ya AFC. Hata hivyo, msimu uliopita haukuwa mzuri kwa timu hii ya jeshi ukilinganisha na msimu wao wa kwanza. JKT Oljoro haina wachezaji wengi wenye majina makubwa lakini lengo lao limekuwa ni kuhakikisha hawashuki daraja huku wakiamini uzoefu wanaoupata utawasaidia kuwa miongoni mwa timu tishio.
MATARAJIO: Watakuwa na wakati mgumu kupigana kuepuka kushuka daraja.

* JKT Ruvu
Msimu uliopita: Nafasi ya 10
Kocha: Mbwana Makata
Waliponea kwenye tundu la sindano kushuka daraja msimu uliopita na safari hii, JKT Ruvu haitataka kurudia makosa hayo. Moja ya sifa kubwa ya JKT Ruvu ni kuzalisha wachezaji wenye vipaja ambao baadaye huvua magwanda na kujiunga na timu za uraiani. Kuondoka kwa kocha Charles Kilinda ambaye inasadikiwa ndiye kocha aliyedumu na timu moja kwa muda mrefu ni pigo kwa JKT Ruvu na sasa wanaanza maisha mapya wakijua fika safari itakuwa ngumu.
MATARAJIO: Kama ilivyokuwa msimu uliopita, kuna kila dalili JKT Ruvu wakawa na wakati mgumu kujinusuru na balaa la kushuka daraja.

* Kagera Sugar
Msimu uliopita: Nafasi ya nne
Kocha: Jackson Mayanja
Kitendo cha kumbakisha mshambuliaji Felix Themi kwa kumuongezea mkataba ni sawa na usajili mpya kwa timu hiyo kwani Themi amekuwa mchezaji muhimu wa Kagera Sugar na ni sawa na nembo ya timu hiyo. Timu hii yenye maskani yake Bukoba imekuwa ikitumia vyema uwanja wake wa Kaitaba. Kocha Mayanja ana jukumu kubwa kuhakikisha moto aliyouwasha Abdallah ‘King’ Kibadeni unaendelea kuwaka.
MATARAJIO: Bado ina safari ndefu ya kuchukua ubingwa ijapokuwa huu ni msimu mwingine tena wa Kagera Sugar kunyanyasa vigogo wa soka nchini

* Mbeya City
Msimu uliopita: Vinara Kundi A
Kocha: Juma Mwambusi
Mara ya mwisho kusikia jina la Juma Mwambusi ni wakati akiwa kocha wa Prisons, ila safari hii anarudi akiwa anaifundisha timu ya Mbeya City aliyoiwezesha kupanda daraja. Mbeya City inaungana na Prisons kuiwakilisha mkoa wa Mbeya. Hii ni moja ya timu ambayo imetabiriwa kuwa na msimu mzuri katika msimu wake wa kwanza.
MATARAJIO: Mbeya City ni miongoni mwa timu ambazo zitamaliza katikati ya ligi.

* Mgambo JKT
Msimu uliopita: Nafasi ya 11
Kocha: Mohammed Kampira
Handeni ni kwao na Uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga ni uwanja wao wa nyumbani. Huu ni msimu wao wa tatu mfululizo Ligi Kuu Bara. Hesabu ndizo zilizowaokoa kuepuka kushuka daraja. Kosa ambalo Mgambo JKT walilofanya msimu uliopita ni kurusu kupoteza idadi kubwa ya michezo yake. Ni dhahiri kocha Kampira atataka safu yake ya ulinzi kuwa makini na washambuliaji kutumia vyema nafasi zitakazotengenezwa.
MATARAJIO: Huu ni mtihani mwingine kwa Mgambo JKT na kuna uwezekano ‘watakuwa wanapumulia mashine’ msimu huu.

* Mtibwa Sugar
Msimu uliopita: Nafasi ya tano
Kocha: Mecky Mexime
Huu ni mwaka wa 13 tangu Mtibwa Sugar kutwaa ubingwa mara ya mwisho na ijapokuwa wamekuwa wakimaliza miongoni mwa nafasi za juu, kiu ya mashabiki ni kuona taji linaenda Turiani mkoani Morogoro. Hazina kubwa ya Mtibwa Sugar ni kutengeneza vipaji ambavyo vimekuwa vikiwatoa udenda timu kubwa. Mshambuliaji wao tegemeo, Hussein Javu, amejiunga na Yanga kumfuata Said Bahanuzi ambaye nyota yake iling’ara akiwa Mtibwa Sugar. Kocha Mexime alivuna pointi sita kutoka kwa Simba na nne kutoka kwa kwa Yanga msimu uliopita na ijapokuwa atataka kurudia mafanikio hayo, mtihani mkubwa ni kuhakikisha asipoteze mechi zingine.
MATARAJIO: Mtibwa Sugar itamaliza kwenye nafasi nne za juu.

* Prisons
Msimu uliopita: Nafasi ya tisa
Kocha: Jumanne Chale
Mechi nyingi walizotoa sare ulichangia kwa kiasi kikubwa Prisons kufanya vibaya msimu uliopita. Timu hii inayomikiliwa na Jeshi la Magereza imekuwa ikijaribu kurudia mafanikio ya 1999 ambapo walifanikiwa kutwaa ubingwa. Namna ambavyo watakavyoanza ligi utakua chachu kwa timu hii kutoka Mbeya kufanya vizuri msimu huu.
MATARAJIO: Bado utakuwa msimu mwingine mgumu kwa Prisons na watahitaji kupambana kuepuka kushuka daraja.

* Rhino Rangers   
Msimu uliopita: Vinara Kundi C
Kocha: Sebastian Nkoma
Mkoa wa Tabora umepata mwakilishi kwenye Ligi Kuu Bara na swali kubwa ni je, watakuwa wamekuja kupapasa na kuondoka? Katika kuonyesha dhamira yao ya kubaki kwenye ligi, Rhino Rangers imemsajili kiungo wa zamani wa Yanga na Simba, Nurdin Bakari. Hii ni fursa nyingine kwa wenyeji wa Tabora kuipa sapoti timu hii yao inayomilikiwa na jeshi.
MATARAJIO: Walikuwa na wakati mzuri Ligi Daraja la Kwanza lakini shughuli ni tofauti Ligi Kuu Bara na vita vyao vitakuwa vya kuepuka kushuka daraja. 

* Ruvu Shooting
Msimu uliopita: Nafasi ya saba
Kocha: Charles Boniface Mkwassa
Hii ni timu ya majeshi ambayo msimu uliopita ndiyo iliyofanya vizuri na sifa lazima zimuende kocha Mkwassa kwani ni mtu anayeweza kuusoma mchezo na kubadilisha timu. Ruvu Shooting imekuwa ikicheza kitimu zaidi na wakati mwingine soka la burudani hususan inapopambana na timu kongwe. Kufanikiwa zaidi kwa Ruvu Shooting kutahitaji kutopoteza katika michezo wanaocheza vizuri.
MATARAJIO: Ni timu ambayo itamaliza kwenye nafasi za katikati.

* Simba
Msimu uliopita: Nafasi ya tatu
Kocha: Abdalla ‘King’ Kibadeni
Unapotaja Simba kwa miaka ya hivi karibuni, huwezi kuitenganisha na majina kama Juma Kaseja na Haruna Moshi ‘Boban’. Lakini hii Simba ya sasa chini ya kocha Kibadeni ina sura mpya huku vijana kama kina Jonas Mkude, Ramadhani Singano na Haruna Chanongo wakipewa nafasi kuonyesha uwezo wao. Maandalizi ya msimu mpya hayakuwa mazuri kwa Simba ila benchi la ufundi lenye watu wazoefu wameshatambua makosa ndani ya timu na kuyafanyia kazi. Simba haitataka kurudia makosa ya msimu uliopita ambapo walianza vizuri lakini wakapoteza mwelekeo na kujikuta katika wakati mgumu kutetea ubingwa wao.
MATARAJIO: Itamaliza katika nafasi tatu za juu na kwasababu haishiriki michuano yoyote ya kimataifa ngazi ya klabu, nguvu zao zote watazielekeza kwenye Ligi Kuu Bara.   

* Yanga
Msimu uliopita: Bingwa
Kocha: Ernie Brandts
Licha ya kumrudisha kundini winga mshambuliaji Mrisho Ngassa, Yanga imehakiksha inabakisha wachezaji wake wa kigeni hususan kiungo mchezeshaji Haruna Niyonzima ambaye alikuwa chachu ya Wanajangwani kutwaa ubingwa. Yanga imekuwa na maandalizi mazuri ya msimu mpya na hilo wamelidhihirisha kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC. Ni dhahiri kuwa hawatataka kuanza vibaya kama walivyofanya msimu uliopita na kazi kubwa aliyonayo kocha Brandts ni kuhakikisha safu yake ya ushambuliaji inayotabiriwa kuwa tishio msimu huu, haipotezi nafasi zitakazo tengenezwa.
MATARAJIO: Kuna uwezekano mkubwa Yanga ikatetea ubingwa wake ila ni Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Yanga safari hii inahitajika kufanya vizuri.

No comments:

Post a Comment