Sekta isiyo rasmi sasa yapata dirisha rasmi la kulinda kesho yake


atika hatua inayotajwa kuwa ni mageuzi makubwa ya kijamii na kiuchumi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Clement Sangu, amezindua rasmi Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya Mwaka 2023 pamoja na Skimu ya Wananchi Waliojiajiri katika Sekta Isiyo Rasmi (Hifadhi Skimu).

Uzinduzi huo uliofanyika jijini Arusha tarehe 9 Februari 2026, unalenga kundi kubwa la Watanzania ambalo kwa muda mrefu lilikuwa nje ya mfumo rasmi wa hifadhi ya jamii.

Akizungumza katika Ukumbi wa Kimataifa wa AICC, Waziri Sangu amebainisha kuwa uzinduzi huo ni mkakati mahususi wa kuwafikia wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo, mama lishe, na waendesha bodaboda. Lengo ni kuhakikisha makundi hayo yanapata ulinzi dhidi ya majanga ya uzee, maradhi, na ulemavu.

"Sera hii inatoa mwelekeo mpya wa utekelezaji wa masuala ya kinga ya jamii nchini, ikienda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inayosisitiza maisha bora kwa wote," alisema Mhe. Sangu. 

Aidha alisema kwamba Serikali imejipanga kuwaandikisha wananchi zaidi ya milioni tano ifikapo Juni 2031 kupitia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Sekta ya Kinga ya Jamii nchini imeshuhudia ukuaji usio wa kawaida katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Takwimu zilizotolewa na Waziri zinaonyesha kuwa:Idadi ya wanachama wa NSSF na PSSSF imeongezeka kutoka milioni 1.5 (mwaka 2020) hadi kufikia milioni 3.1 (Desemba 2025), sawa na ongezeko la asilimia 106.

Pia amesema uwekezaji wa mifuko umekua hadi kufikia Shilingi trilioni 20.13 na kufanya thamani ya  mifuko yote kwa pamoja sasa imegusa Shilingi trilioni 24.20.

Habari njema zaidi ni kuwa kuanzia Julai 2025 wastaafu wameboreshewa  pensheni kutoka Shilingi laki moja hadi laki mbili na nusu huku malipo yakifanyika kila tarehe 25 ya mwezi.

Mbali na mifuko ya uchangiaji, Serikali imeendelea kuimarisha ustawi wa kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Waziri Sangu amefafanua mafanikio ya awamu mbili za mpango huo.

Awamu ya Kwanza ilinufaisha kaya milioni 1.1 kwa huduma zenye thamani ya Shilingi bilioni 968 wakati Awamu ya Pili (2020–2025), zaidi ya kaya milioni 1.37 zenye watu takribani milioni 5.5 zimenufaika.

Katika kipindi hicho Serikali imetoa ruzuku ya zaidi ya Shilingi trilioni 1.55, huku mpango wa ajira za muda ukiwanufaisha walengwa laki sita (600,000) kwa ujira wa zaidi ya Shilingi bilioni 214. Hatua hizi zimetajwa kuimarisha ustahimilivu wa familia nyingi dhidi ya majanga ya kiuchumi.

Uzinduzi wa Sera ya mwaka 2023 unadhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma. 

No comments