Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo, kikao cha Kamati ya Ufundi, kilichoketi Mei 11 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Harbours Club, chini ya Mwenyekiti wa kamati hiyo, Joseph Kanakamfumu, alisema kozi ya ualimu wa mpira wa miguu ngazi ya cheti (Inter-Mediate), ambayo imekuwa kwenye mahitaji makubwa, itaanza Juni 3 hadi 28 mwaka huu.
Kozi itakuwa kwa siku 10, tunatarajia kupata washiriki watakaofikia 60, iwapo idadi hiyo itafikia na kuzidi, kutakuwa na awamu mbili za wanafunzi ambao kisheria darasa linatakiwa kuwa na wanafunzi 35 hadi 40.
Watu wataanza kujiandikisha kuanzia Mei 15 hadi 26 na awamu ya kwanza ya kozi itaanza Juni 3 hadi 14 na ya pili itaanza Juni 17 hadi 28.
Ada ya ushiriki itakuwa Sh 50,000 na itahusisha gharama ya kuchukulia fomu 5,000 na zilizobaki ni gharama ya cheti, kitambulisho pamoja na chakula cha mchana.
Kwa upande wa kozi ya waamuzi itaanza Septemba 3 hadi 9 mwaka huu na ada itakuwa Sh 25, 000.
Fomu zitapatikana katika ofisi za Mikoa ya kisoka, TEFA, IDFA,KIFA na DRFA na kozi zote zitafanyika kwenye ukumbi wa Harbours Club.
Kamati hiyo imepanga kukutana Mei 19 kwenye Ukumbi huo wa Harbours Club saa tatu asubuhi na viongozi wote wa timu za wanawake kutathimini michango yao kwa ukuzaji wa soka la Wanawake wa mkoa wa Dar es Salaam.
Wajumbe waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya DRFA, Kennedy Mwaisabula, Jovin Ndimbo (Mwenyekiti Kamati ya Waamuzi), Benny Kisaka (Mwenyekiti Kamati ya Soka la Wanawake), Abdallah Mitole (Mjumbe kamati ya waamuzi), Sijali Juma (Mjumbe kamati ya waamuzi), Richard Mbuya (Mjumbe kamati ya Soka la Wanawake) na Dk. Maneno Tamba (Mjumbe Kamati ya Soka la Wanawake)
No comments:
Post a Comment