Vita kusaka tiketi ya kusafiri kwenda jijini London kwenye mchezo wa fainali wa klabu bingwa barani Ulaya inaanza usiku huu kati ya Mabingwa wa soka nchini Ujerumani dhidi ya inayotajwa kuwa timu bora kwa vilabu vya soka duniani kwa wakati huu FC Barcelona.
Kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes amesema haogopeshwi na urejeo wa nyota wa Barcelona, Lionel Messi kuelekea mchezo huo wa kwanza wa nusu fainali ya klabu bingwa barani Ulaya.

Messi hajacheza mchezo wowote wa Barcelona toka alipoingia kama mchezaji wa akiba na kuisaidia timu yake kufuzu nusu fainal katika mchezo robo fainali dhidi ya Paris St-Germain ya Ufaransa. Lakini kuna kila dalili Muanjetina huyo mwenye umri wa miaka 25 ambaye ndiye mchezaji bora wa dunia kwa sasa,akajumuishwa kwenye kikosi cha Barcelona kwenye mchezo wa usiku wa leo.

Mwezi uliopita Messi aliweka rekodi kwenye ligi ya Hispania kwa kuwa mchezaji aliyezifunga timu zote zinazoshiriki ligi kuu nchini humo maarufu kama La Liga kwa misimu miwili mfululizo.
Barcelona inapambana kutaka kutwaa taji la tatu la klabu bingwa barani Ulaya ndani ya miaka mitano,Huku Bayern Munich ambao msimu ujao watakuwa chini ya aliyekuwa kocha wa Barcelona, Pep Guardiola, wao wanapambana kutafuta nafasi ya kucheza fainali yao ya tatu ndani ya miaka minne