Na Rahel Pallangyo
TIMU ya soka ya wanawake ya Tanzania Bara chini ya umri wa miaka 18 imetwaa ubingwa wa mashindano ya Cecafa baada ya kuifunga Uganda kwa bao 1-0 katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam jana.
Tanzania Bara ilianza mchezo kwa kasi wakilazimisha kupata bao la mapema lakini walisubiri hadi dakika ya 43, Koku Kipanga alipopiga shuti kwa mpira wa adhabu na kugonga mwamba ukarejea uwanjani na Winfrida Gerald akaumalizia na kufunga bao na kuibua nderemo kwa mashabiki waliojaza uwanja pomoni.
Licha ya kupata bao Bara walionesha kuwa na kiu ya kuongeza bao zaidi na kuendelea kushambuliana kwa zamu na Uganda na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ndogo kila timu ikijitahidi kupanga mashambulizi na Uganda waliliandama lango la Bara karibu dakika 30 za mwanzo wa kipindi cha pili lakini safu ya mabeki iliyokuwa na wachezaji watano iliwadhibiti vema.
Licha ya Uganda kufanya mabadiliko mengi kipindi cha pili walishindwa kuharibu mbinu za kocha Bakari Shime aliyekuwa akitumia mfumo wa 5:1:3:1 na wao wakitumia mfumo wa 4:4:2:1 kwani hadi filimbi ya mwisho ya mwamuzi Suavis Iratunga kutoka Burundi Bara walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Kwa matokeo hayo Tanzania Bara ndio bingwa wa kwanza wa mashindano ya umri huo ikiwa na pointi 12 ikifuatiwa na Uganda iliyomaliza na pointi tisa, nafasi ya tatu ilikwenda kwa Ethiopia yenye pointi sita, Burundi ikashika nafasi ya nne kwa pointi tatu baada ya kuifunga Zanzibar kwa mabao 4-0 katika mchezo uliochezwa mapema saa tisa alasiri.
Kwa upande wa mfungaji bora ni Emush Daniel wa Ethiopia alifunga mabao matano akifuatiwa na mshambuliaji wa Tanzania Bara, Aisha Mnuka aliyefunga mabao matatu.
Mashindano haya yalianza kutimua vumbi Julai 25, mwaka huu yakichezwa kwa mtindo wa ligi kwani yanashirikisha timu tano baada ya Rwanda na Kenya kujitoa.
Mwisho
No comments:
Post a Comment